Oct 22, 2019 07:58 UTC
  • AU: Ebola imeua watu 2,150 kufikia sasa Kongo DR

Umoja wa Afrika umesema idadi ya watu walioaga dunia katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa homa hatari ya Ebola imefikia 2,150 tangu maradhi hayo yaripuke tena katika nchi hiyo Julai mwaka jana.

Takwimu mpya za Taasisi ya Kupambana na Kudhibiti Magonjwa ya Umoja wa Afrika (Africa CDC) imesema idadi ya watu walioaga dunia kutokana na ugonjwa wa Ebola nchini DRC sasa imefikia 2,150. Mwanzoni mwa mwezi huu, idadi hiyo ilikuwa 2,133 lakini baadaye hadi kufikia Oktoba 13, idadi hiyo iliongezeka na kufikia 2,150.

Wakati huohuo, mawaziri wa afya wa nchi tisa jirani na Kongo DR na maafisa wa ngazi za juu wa uhamiaji wa nchi hizo wamekutana mjini Goma, mashariki  mwa DRC kujadili mikakati ya kupambana na jinamizi hilo la Ebola.

Mkutano huo umehudhuriwa pia na wawakilishi wa taasisi za kimataifa likiwemo Shirika la Afya Duniani WHO na Umoja wa Afrika,

Chanjo ya Ebola

Katika kikao hicho, mawaziri hao wamepasisha kwa kauli moja kuwa, serikali zao zitaunda Jopokazi la Uratibu wa Ebola Afrika (AfECT), ambalo litakuwa na jukumu la kufanikisha ushirikiano katika vita dhidi ya ugonjwa huo hatari.

Ikumbukwe kuwa, mripuko mkubwa zaidi wa ugonjwa hatari wa Ebola ulitokea baina ya Disemba 2013 na Aprili 2016 na kuua zaidi ya watu 11,000 katika nchi za Guinea, Liberia na Sierra Leone huko magharibi mwa bara la Afrika.

Tags