Mvua na mafuriko yaendelea kuua na kusababisha hasara nchini Tanzania
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i56871-mvua_na_mafuriko_yaendelea_kuua_na_kusababisha_hasara_nchini_tanzania
Mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali ya Tanzania zimeendelea kusababisha maafa na hasara kubwa nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 26, 2019 08:38 UTC
  • Mvua na mafuriko yaendelea kuua na kusababisha hasara nchini Tanzania

Mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali ya Tanzania zimeendelea kusababisha maafa na hasara kubwa nchini humo.

Watu wanane wamefariki dunia usiku wa kuamkia leo Jumamosi, baada ya gari aina ya Noah walilokuwa wakisafiria kutumbukia mtoni katika eneo la Sindeni barabara kuu ya Handeni Korogwe, kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha. 

Vifo hivyo vimesababisha idadi ya watu waliofariki dunia kutokana na mvua hizo kuongezeka na kufikia watu 37 kutoka 29 iliyotangazwa siku chache zilizopita na Kamanda wa Polisi mkoa wa Tanga, Edward Bukombe.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Edward Bukombe amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema kuwa ajali hiyo imetokea wakati wasafiri wakitoka Handeni kwenda Tanga Mjini.

Mafuriko Zanzibar. Mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika maeneo ya kaskazini mwa Misri zimeshaua watu 20 hadi hivi sasa

Mamia ya abiria waliokuwa wanasafiri kutoka Arusha, Kilimanjaro na nchi jirani na waliotoka Dar es Salaam kuelekea mikoa mbalimbali wamekwama tangu jana mchana Ijumaa wilayani Korogwe na Handeni Mkoa wa Tanga kutokana na mafuriko hayo.

Katika nchi jirani ya Kenya,  watu 29 wameshapoteza maisha yao kufikia sasa kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo tofauti ya nchi hiyo.

Wakati huohuo, Ofisi ya Uratibu ya Umoja wa Mataifa Inayoshughulikia Masuala ya Kibinaadamu (OCHA) imeripoti kuwa, watu zaidi ya laki 9 wakiwemo wakimbizi wamepoteza makazi yao au kuathirika kwa njia moja au nyingine na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa zinaoendelea kunyesha katika maeneo ya kaskazini mwa Sudan Kusini.