Wakimbizi 180 watiwa mbaroni nchini Afrika Kusini
Polisi wa Afrika Kusini wamewatia nguvu zaidi ya wakimbizi 180 wa nchi za kigeni baada ya kufanya maandamano ya kulalamikia hali yao mbaya.
Taarifa ya jeshi la polisi la Afrika Kusini imesema kuwa, watu hao raia wa kigeni wamekamatwa kwa kosa la kushambulia ofisi ya Kamishna Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) wakati walipokuwa wanashinikiza kupewa vibali vya kwenda nchi nyingine.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, tarehe 8 Oktoba raia hao wa kigeni waliteka njia za watu wanaotembea kwa miguu mbele ya ofisi za UNHCR ili kulishinikiza shirika hilo liwasaidie kuondoka Afrika Kusini na kwenda nchi nyingine.
Wakimbizi hao wanasema kuwa hali yao ya kiusalama ni mbaya sana nchini Afrika Kusini kutokana na kushambuliwa na wenyeji wa nchi hiyo wanaochukia wageni.
Itakumbukwa kuwa watu 12 waliuawa mwezi Septemba 2019 baada ya kutokea fujo zilizosababishwa na wenyeji wa Afrika Kusini ambao wanachuki na wageni.
Waafrika Kusini hao wanadai kuwa wageni wamevamia nchi yao na kuteka nafasi zao za ajira na kuwasababishia matatizo ya kimaisha wenyeji wa nchi hiyo.
Machafuko ya mwezi Septemba yalipelekea kuingia doa uhusiano wa Afrika Kusini na nchi nyingine kiasi kwamba Nigeria iliamua kuwaita nyumbani raia wake kutoka Afrika Kusini huku raia wa Nigeria nao wakishambulia maeneo ya raia wa Afrika Kusini nchini Nigeria ili kulipiza kisasi.