Dec 10, 2019 12:02 UTC
  • Mahakama ya Algeria yawahukumu kifungo jela mawaziri wakuu wawili wa zamani

Mahakama ya Sidi M'Hamed katika mji mkuu wa Algeria, Algiers imewahukumu vifungo vya muda mrefu jela mawaziri wakuu wawili wa zamani wa nchi hiyo baada ya kupatikana na hatia zinazohusiana na ufisadi na ubadhirifu wa mali ya umma.

Ahmed Ouyahia amehukumiwa kifungo cha miaka 15 na faini ya dola 16,000 na Abdelmalek Sellal kifungo cha miaka 12 jela na faini ya dola 8,000 kwa kupatikana na hatia zinazohusiana na ufisadi na kuchangia kwa siri kampeni za rais aliyejiuzulu wa nchi hiyo, Abdelaziz Bouteflika.

Vilevile jaji wa kesi hiyo iliyotajwa na vyombo vya habari vya Algeria kuwa ni ya kihistoria, ameamuru kutaifishwa mali na milki zote za Ouhahia na Sallal.

Mahakama hiyo pia imemhukumu kifungo cha miaka 20 jela waziri wa zamani wa viwanda wa Algeria, Abdeslam Bouchouareb bila yaye kuwepo mahakamani na imeitaka Polisi ya Kimataifa kumtia nguvuni.

Mawaziri wengine wa zamani watatu wa Algeria pia wamehukumiwa vifungo vya baina ya miaka 5 hadi kumi kwa hatia zinazohusiana na ufisadi, rushwa, kutumia vibaya madaraka na kupata utajiri kwa njia zisizo za kisheria.

Mahakama ya Mahakama ya Sidi M'Hamed, Algiers

Baadhi ya watu waliokuwa wamekusanyika nje ya Mahakama ya Sidi M'Hamed mjini Algiers walishangilia na kupongeza uamuzi huo.

Hii ni mara ya kwanza kuhukumiwa waziri mkuu wa zamani nchini Algeria tangu nchi hiyo ilipopata uhuru mwaka 1962.

Tags