Mawaziri wanne wa Ulaya kutembelea Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i58169-mawaziri_wanne_wa_ulaya_kutembelea_libya
Serikali ya Muafaka wa Kitaifa Libya imetangaza kuwa, mawaziri wa mambo ya nje wa Italia, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani wanatazamiwa kutembelea mji mkuu wa nchi hiyo, Tripoli.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 28, 2019 23:23 UTC
  • Mawaziri wanne wa Ulaya kutembelea Libya

Serikali ya Muafaka wa Kitaifa Libya imetangaza kuwa, mawaziri wa mambo ya nje wa Italia, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani wanatazamiwa kutembelea mji mkuu wa nchi hiyo, Tripoli.

Kwa mujibu wa  Televisheni ya Roosiya Al Youm, Mohamed Taher Siala Waziri wa Mambo ya Nje wa Libya, amefanya mazungumzo ya simu na Joseph Borrel, mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya. Imedokezwa kuwa wawili hao wamejadili kuhusu matukio ya sasa ya Libya na namna ambavyo jenerali muasi Khalifa Haftar, kamanda wa wanamgambo wanaojiita, 'Jeshi la Kitaifa la Libya' anavyotekeleza jinai dhidi ya watu wa miji kadhaa ya Libya ukiwemo Tripoli mji mkuu wa nchi hiyo.

Katika mazungumzo hayo, Borell amesema kuwa, mnamo Januari 7, akiwa ameandamana na mawaziri wa mambo ya nje wa Italia, Ujerumani, Uingereza na Ufaransa watafika mjini Tripoli kwa ajili ya kuonana na kufanya mazungumzo na Fayez al-Sarraj, Waziri Mkuu wa Serikali ya Muafaka wa Kitaifa na wakuu wengine wa nchi hiyo.

 Fayez al-Sarraj, Waziri Mkuu wa Serikali ya Muafaka wa Kitaifa Libya

Hayo yanaripotiwa katika hali ambayo wanamgambo wanaoongozwa na Haftar ambaye anapata uungaji mkono wa kifedha na kisilaha kutoka Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu walianzisha hujuma dhidi ya Tripoli mwezi Aprili mwaka huu.

Kufuatia hali hiyo, Serikali ya Muafaka wa Kitaifa ya Libya imeomba rasmi msaada wa kijeshi kutoka Uturuki ili kukabiliana na wanamgambo hao. Uturuki imekubali ombi hilo, jambo ambalo limeibua wasiwasi mkubwa kuhusu uwezekano wa kuenea wigo wa vita vya Libya.