Arab League yaonya juu ya kutumwa majeshi ajinabi Libya
(last modified Wed, 01 Jan 2020 08:00:33 GMT )
Jan 01, 2020 08:00 UTC
  • Arab League yaonya juu ya kutumwa majeshi ajinabi Libya

Jumuiya ya Nchi za Kiarabu imeziasa pande hasimu za kisiasa nchini Libya kujiepusha na hatua yoyote ambayo itachochea kutumwa vikosi vya nchi za kigeni katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Baraza Kuu la Arab League limeitisha mkutano wa dharura katika mji mkuu wa Misri, Cairo wa kujadili hali ya Libya, wakati huu ambapo kundi la wapiganaji linalojiita Jeshi la Taifa la Libya chini ya uongozi wa jenerali mstaafu wa jeshi Khalifa Haftar, linaendeleza mashambulizi yake ya kutaka kudhibiti mji mkuu Tripoli.

Taarifa ya mkutano huo wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu imeonya kuwa, "Hatua ya upande mmoja itakayopelekea kutumwa vikosi ajinabi nchini Libya haitakuwa na tija nyingine ghairi ya kushadidisha mgogoro unaolikumba taifa hilo."

Hii ni katika hali ambayo, serikali ya Uturuki imetangaza baada ya kusaini mapatano mawili na serikali ya umoja wa kitaifa chini ya uongozi wa Waziri Mkuu Fayez al Sarraj inayoungwa mkono na jamii ya kimataifa kwamba, iko tayari kutuma wanajeshi wake Libya kwa ajili ya kurejesha usalama nchini humo. Bunge la Uturuki wiki hii linatazamia kujadili kibali cha kutumwa wanajeshi wa nchi hiyo huko Libya. 

Rais wa Uturuki na Fayez al-Sarraj wakiongoza mkutano wa pande mbili Tripoli

Hii ni katika hali ambayo, Misri ambayo hivi sasa inatunishiana misuli ya kidiplomasia na Uturuki imekuwa ikisisitiza kuwa ipo tayari pia kutuma wanajeshi wake nchini Libya kwenda kushirikiana na vikosi vya Khalifa Haftar.

Libya haijashuhudia amani na imekuwa ikikumbwa na hali ya mchafukoge tangu baada ya kupinduliwa serikali ya mtawala dikteta kanali Muammar Gaddafi mwaka 2011.