Watu 36 wauawa katika mapigao ya kikabila Darfur, Sudan
(last modified Wed, 01 Jan 2020 08:12:59 GMT )
Jan 01, 2020 08:12 UTC
  • Watu 36 wauawa katika mapigao ya kikabila Darfur, Sudan

Kwa akali watu 36 wameuawa katika mapigano ya kikabila yanayoendelea kushuhudiwa katika mkoa wa Darfur Magharibi nchini Sudan.

Duru za hosiptali na maafisa wa serikali katika eneo hilo wamesema, miongoni mwa makumi ya watu waliouawa katika mapigano hayo ya jana Jumanne baina ya Waarabu na wasiokuwa Waarabu ni wanawake na watoto wadogo, na kwamba watu wengine 60 wamejeruhiwa.

Habari zaidi zinasema kuwa, majeruhi 49 wamepelekwa katika mji mkuu Khartoum kwa ajili ya matibabu. 

Adam Regal, msemaji wa shirika moja la kuwasaidia wakimbizi katika eneo hilo amesema kambi tatu za wakimbizi katika mji wa Genena zimeshambuliwa huku mali ya thamani kubwa zikiharibiwa kwa kuteketezwa moto.

Wapiganaji wa kikabila katika eneo la Darfur Magharibi

Serikali mpya ya Sudan imeahidi kumaliza migogoro nchini humo ukiwemo ule wa Darfur ambao umepelekea watu wasiopungua laki tatu kuuawa na wengine milioni mbili na nusu kuwa wakimbizi tangu mwaka 2003.

Mwishoni mwa mwezi uliomalizika wa Disemba, maafisa 51 wa utawala ulioondolewa madarakani nchini humo wa Omar al-Bashir walitiwa nguvuni baada ya Mwendesha Mashtaka Mkuu kuwatuhumu kwamba walihusika na uhalifu ikiwa ni pamoja na jinai dhidi ya binadamu katika eneo la Darfur.