28 wauawa katika shambulizi dhidi ya kambi ya jeshi Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i58319-28_wauawa_katika_shambulizi_dhidi_ya_kambi_ya_jeshi_libya
Kwa akali watu 28 wameuawa katika shambulizi la anga lililolenga chuo cha kijeshi katika mji mkuu wa Libya, Tripoli.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 05, 2020 04:11 UTC
  • 28 wauawa katika shambulizi dhidi ya kambi ya jeshi Libya

Kwa akali watu 28 wameuawa katika shambulizi la anga lililolenga chuo cha kijeshi katika mji mkuu wa Libya, Tripoli.

Hamid bin Omar, Waziri wa Afya ya Serikali ya Muafaka wa Kitaifa Libya (GNA) inayoongozwa na Waziri Mkuu Fayez al-Sarraj ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, idadi ya wahanga wa shambulizi hilo la jana jioni dhidi ya kituo cha kijeshi cha Al-Hadhba mjini Tripoli yumkini ikaongezeka.

Msemaji wa shirika la ambulensi la Tripoli, Osama Ali amesema miili imetapakaa katika barabara ya As Sidra katikati mwa Tripoli kufuatia shambulizi hilo la anga. 

Inaaminika kuwa, wapiganaji wanaojiita 'Jeshi la Kitaifa la Libya' ndio wametekeleza hujuma hiyo, ingawaje msemaji wa wanamgambo hao wanaoongozwa na jenerali muasi Khalifa Haftar amekanusha madai hayo.

Jenerali muasi Khalifa Haftar

Wapiganaji wa Khalifa Haftar mwezi Aprili mwaka uliopita wa 2019 walianzisha mashambulizi ya kutaka kuudhibiti mji mkuu, Tripoli.

Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, watu zaidi ya 2,000 wakiwemo raia 280 wameuawa jijini Tripoli na wengine wasiopungua 140,000 wamejeruhiwa tangu kuanza mashambulizi hayo ya kundi la wanamgambo wa Haftar, wanaoungwa mkono na Saudi Arabia, Marekani, Imarati na baadhi ya nchi za Ulaya kama Ufaransa.