Fayez al-Sarraj azitaka pande hasimu Libya kufanya suluhu
Waziri Mkuu wa Serikali ya Maridhiano ya Kitaifa ya Libya, Fayez al-Sarraj amezitaka pande zinazoshiriki katika mapigano kufikia suluhu.
Al-Sarraj amesema, anawataka Walibya kusahau yaliyopita, kuachana na tofauti zao na kuungana pamoja kuelekea kwenye usalama na amani. Amedai kwamba anakusudia kuzuia umwagikaji zaidi wa damu ya raia wa Libya. Wakati huo huo serikali ya maridhiano ya kitaifa ya Libya imetangaza kwamba Fayez al-Sarraj amefanya mazungumzo na Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki kuhusiana na makubaliano ya hivi karibuni ya ushirikiano wa kuisalama pamoja na masuala ya baharini kati ya nchi mbili. Katika hatua nyingine Jenerali Muasi Khalifa Haftar anayeongoza kundi linalojiita 'Jeshi la Kitaifa la Libya' amefanya safari nchini Russia kwa ajili ya kufanya mazungumzo na viongozi wa nchi hiyo.
Hii ni katika hali ambayo Jumamozi iliyopita Haftar alitangaza kukubali pendekezo la Russia na Uturuki kwa ajili ya usitishaji vita nchini Libya. Usitishaji vita huo ulianza kutekelezwa asubuhi ya jana, ingawa hata hivyo pande mbili zimetuhumiana kwa uvunjwaji wa usitishaji mapigano huo. Kwa sasa Libya imegawanyika sehemu mbili za kiutawala, ambapo moja ni inadhibitiwa na serikali ya umoja wa kitaifa yenye makao yake mjini Tripoli na inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa, huku nyingine ikiwa na mako makuu yake mjini Tobruk chini ya usimamizi wa Khalifa Haftar ambayo pia inaungwa mkono na Saudia, Imarati, Misri na nchi kadhaa za Magharibi ikiwemo Marekani.