Magaidi 17 waangamizwa katika mkoa wa Sinai, Misri
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Misri imetangaza habari ya kuuawa wanachama 17 wa genge moja la kigaidi katika mji wa al-Arish, katika mkoa wa Sinai Kaskazini.
Taarifa ya jana usiku ya wizara hiyo imesema, magaidi hao wameangamizwa katika operesheni ya jeshi la Misri katika eneo la al-Ubaidat mjini al-Arish katika mkoa wa Sinai Kaskazini unaoshudia hali ya mchafukoge kwa muda mrefu sasa.
Mkoa wa Sinai wa kaskazini mwa Misri umekuwa uwanja wa mapigano baina ya maafisa usalama na magenge ya kigaidi ambayo yameshadidisha mashambulizi yake katika miaka ya hivi karibuni, hususan baada ya mapinduzi ya kijeshi yaliyoiondoa madarakani serikali halali ya nchi hiyo iliyokuwa ikiongozwa na Mohammad Morsi hapo mwaka 2013.
Utawala wa sasa wa Rais Abdul Fattah al-Sisi umekuwa ukikosolewa vikali na wananchi wa Misri kutokana na ukosefu wa usalama na kushtadi mashambulizi ya magenge ya kigaidi katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
Makundi ya kigaidi hususan lile linalojiita Wilaya ya Sinai yamekuwa yakifanya hujuma na mashambulizi ya mara kwa mara nchini Misri hususan katika mkoa wa Sinai Kaskazini.