Waziri wa zamani wa Algeria kuwa mjumbe maalumu wa UN nchini Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i59693-waziri_wa_zamani_wa_algeria_kuwa_mjumbe_maalumu_wa_un_nchini_libya
Waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Algeria ametangazwa kuwa chaguo la baadae la kushika nafasi ya mjumbe wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Libya.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Mar 12, 2020 04:26 UTC
  • Waziri wa zamani wa Algeria kuwa mjumbe maalumu wa UN nchini Libya

Waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Algeria ametangazwa kuwa chaguo la baadae la kushika nafasi ya mjumbe wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Libya.

Duru za kidiplomasia zimesema kuwa, Ramtane Lamamra, waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Algeria ndiye atakayeshika nafasi ya Ghassan Salamé, mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Libya.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria,  Sabri Boukadoum, amesema ana matumaini kuwa mjumbe maalumu mpya wa Umoja wa Mataifa nchini Libya atatangazwa karibuni hivi na inabidi mtu huyo awe anakubaliwa na pande zote hasimu huko Libya.

Ghassan Salamé hivi karibuni alipeleka barua ya kujiuzulu baada ya kuwa mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Libya kwa muda wa miaka mitatu. Amesema, afya yake haimruhusu kuendelea na purukushani za upatanishi wa mgogoro mgumu wa Libya.

Ghassan Salamé

 

Hata hivyo pande hasimu nchini Libya zinamlaumu Ghassan Salamé kutokana na msimamo wake wa kutangaza kuanza mazungumzo ya Libya katika michakato mitatu ya kisiasa baada ya mazungumzo ya amani ya Berlin.

Mgogoro wa Libya ulipamba moto sana tangu mwezi Aprili 2019 baada ya jenerali muasi Khalifa Haftar kuanzisha mashambulizi ya pande zote dhidi ya mji mkuu wa nchi hiyo, Tripoli.

Jenerali huyo muasi anayeongoza kundi linalojiita "Jeshi la Taifa la Libya" anaungwa mkono na nchi kama Saudi Arabia, Misri na Umoja wa Falme za Kiarabu.

Juhudi za kimataifa za kurejesha amani nchini Libya kupitia mazungumzo baina ya pande hasimu hadi hivi sasa zimeshindwa kuzaa matunda ya maana.