Watoto 3 wauawa katika shambulizi la wapiganaji wa Haftar Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i59835-watoto_3_wauawa_katika_shambulizi_la_wapiganaji_wa_haftar_libya
Watoto watatu wa familia moja wameuawa baada ya kundi la wanamgambo kwa jina la jeshi la kitaifa la Libya linaloongozwa na Jenerali muasi Khalifa Haftar kulishambulia kwa mabomu eneo la Ain Zara, kusini mwa mji mkuu wa Libya, Tripoli.
(last modified 2026-03-17T04:36:21+00:00 )
Mar 19, 2020 04:22 UTC
  • Watoto 3 wauawa katika shambulizi la wapiganaji wa Haftar Libya

Watoto watatu wa familia moja wameuawa baada ya kundi la wanamgambo kwa jina la jeshi la kitaifa la Libya linaloongozwa na Jenerali muasi Khalifa Haftar kulishambulia kwa mabomu eneo la Ain Zara, kusini mwa mji mkuu wa Libya, Tripoli.

Hayo yamesemwa na Amin Hashem, Mshauri wa Habari wa Wizara ya Afya ya Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa, na kuongeza kuwa, roho za watoto wa Libya zinaendelea kupotea kufuatia kushadidi hali ya ukosefu wa usalama katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Hii si mara ya kwanza kwa wanamgambo wa Khalifa Haftar kushambulia eneo la makazi ya watu na kuua raia wasio na hatia, ingawaje mara zote wamekuwa wakikanusha kuhusika na hujuma hizo.

Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) umetahadharisha kwamba, mashambulio ya kiholela dhidi ya makazi ya raia nchini Libya yameifanya hali ya watoto na raia nchini humo izidi kuwa mbaya.

Jenerali Khalifa Haftar, kiongozi wa wanamgambo wa Libya wanaojiita Jeshi la Taifa

Mapema mwezi huu, UNICEF ilitangaza kuwa, watu wasiopungua 1,800,000 wameathirika vibaya na vita vya ndani nchini humo ambapo 266,000 kati yao ni watoto wadogo.

Tokea Aprili mwaka jana wakati Jenerali Khalifa Haftar alipoanzisha vita dhidi ya mji mkuu Tripoli, maelfu ya watu wameuawa na kujeruhiwa, mbali na wengine 150,000 kuachwa bila makao.