Maafisa usalama wa Msumbiji waua magaidi 50 Cabo Delgado
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i60996
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Msumbiji amesema maafisa usalama wa nchi hiyo wamefanikiwa kuwaangamiza magaidi 50 ndani ya siku chache zilizopita katika eneo la kaskazini la Cabo Delgado.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
May 15, 2020 12:26 UTC
  • Maafisa usalama wa Msumbiji waua magaidi 50 Cabo Delgado

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Msumbiji amesema maafisa usalama wa nchi hiyo wamefanikiwa kuwaangamiza magaidi 50 ndani ya siku chache zilizopita katika eneo la kaskazini la Cabo Delgado.

Amade Miquidade alisema hayo jana Alkhamisi katika kikao na waandishi wa habari na kuongeza kuwa, "Mei 13 (juzi Jumatano), magadii waliviziwa na askari wetu katika makutano ya barabara inayounganisha Chinda na Mbau, ambapo 42 waliuawa."

Amebainisha kuwa, maafisa usalama wa nchi hiyo ya kusini mwa Afrika jana Alkhamisi walifanikiwa kuwaua magaidi wengine wanane katika wilaya ya Quissanga, mkoani Cabo Delgado.

Amesema lengo la magaidi hao ni kuvurugaamani na usalama, na kuwakatisha tamaa watu wa jamii za nchi hiyo sambamba na kupanda mbegu za chuki baina yao.

Hivi karibuni jeshi la polisi nchini Msumbiji lilitangaza habari ya kuuawa makumi ya watu katika shambulizi jipya la kigaidi lililotokea huko kaskazini mwa nchi hiyo ya kusini mwa Afrika.

Maafisa usalama mkoani Cabo Delgado

Uasi wa wanamgambo nchini Msumbiji umeibuka na kuwa vita vya wazi katika wiki za hivi karibuni, huku kukiwa na ripoti za mauaji, watu kukatwa vichwa na kutekwa kwa miji miwili katika mkoa wa kaskazini wa Cabo Delgado.

Vijiji vya mkoa huo wa Cabo Delgado ulioko kaskazini mwa Msumbiji tangu mwezi Oktoba mwaka 2017 vimekuwa vikishuhudia mashambulizi ya umwagaji damu ya wanachama wa kundi linalojiita Ahlu Sunna Wal Jamaa, ambao wakazi wa maeneo hayo wanawatambua kwa jina la al-Shaabab.