Wanachama kadhaa wa al-Shabaab waangamizwa na jeshi la Jubaland
(last modified Tue, 26 May 2020 02:27:25 GMT )
May 26, 2020 02:27 UTC
  • Wanachama kadhaa wa al-Shabaab waangamizwa na jeshi la Jubaland

Jeshi la eneo lenye mamlaka ya ndani la Jubaland limetangaza habari ya kuangamiza wanachama wanne wa kundi la kigaidi na ukufurishaji la al-Shabaab katika mji wa Dhobley, Kusini mwa Somalia.

Mohamed Abdullahi, Naibu Kamanda wa Jeshi la Polisi la eneo hilo amesema magaidi hao wa al-Shabaab waliuawa katika makabiliano ya jana Jumatatu na vikosi vya eneo hilo lenye mamlaka ya ndani, kusini mwa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika. Mfumo wa utawala Somalia ni wa kifiderali ambapo majimbo kadhaa nchini humo yana mamlaka ya ndani ya kujitawala.

Kamanda huyo wa Jeshi la Polisi la Jubaland amefafanua kuwa, "wapiganaji wenye misimamo mikali wa al-Shabaab walivamia kituo cha mafunzo cha vikosi vya Jubaland na kupelekea kutokea makabiliano makali baina ya jeshi na wavamizi. Tumeua wanachama wanne wa kundi hilo katika mapigano hayo, wengine wametoroka nje ya mji na hivi sasa vikosi vyetu vinaidhibiti kambi hiyo."

Shambulizi hili linajiri siku tatu baada ya wanachama wengine wa kundi la kigaidi la al-Shabaab kuangamizwa na maafisa usalama katika mji wa Burdhubo, unaopatikana katika eneo la Gedo, kusini mwa Somalia.

Wanachama wa al-Shabaab wanaoendeleza harakati za kikatili Somalia

Kadhalika haya yanaripotiwa masaa machache baada kujiri mripuko wa bomu katika mji wa Baidoa, kusini mwa nchi hiyo, na inasadikika kuwa genge hilo la ukufurishaji ndilo lililohusika na ukatili huo.

Kwa mujibu wa ripoti, bomu hilo liliripuka usiku wa kuamkia jana Jumatatu wakati wa sherehe za Idul-Fitr katika mji huo, ambapo watu watano waliuawa na wengine 20 kujeruhiwa.

 

 

Tags