Jeshi la Somalia laangamiza magaidi 37 wa al-Shabaab
Jeshi la Taifa la Somalia limetangaza kuwa limefanikiwa kuua makumi ya wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab huko kusini mwa nchi.
Odawa Yusuf Rage, kamanda mwandamizi wa jeshi hilo alisema hayo jana Jumapili na kuongeza kuwa, magaidi 37 wa al-Shabaab waliuawa Jumamosi baada ya kujiri makabiliano makali baina ya pande mbili hizo katika mji wa Hudur, eneo la Bakol kusini mwa nchi.
Amesema jeshi la Somalia limetwaa silaha zilizokuwa mikononi mwa magaidi hao. Hata hivyo hajatoa maelezo yoyote iwapo askari wa serikali wameuawa au kujeruhiwa kwenye makabiliano hayo au la.
Hii ni katika hali ambayo, wakazi wa kijiji cha Abal, mjini Hudur, eneo la Bakol kusini mwa Somalia wamesema pande zote mbili zimepata hasara kubwa katika makabaliano hayo.
Mwishoni mwa mwezi uliopita wa Mei, genge hilo la ukufurishaji liliuawa wanajeshi 14 wa Somalia katika mashambulizi mawili ya mabomu katika maeneo ya Juba ya Kati na Lower Shebelle.
Kundi la kigaidi a kitakfiri la al-Shabaab lenye mfungamano na mtandao wa kigaidi wa al-Qaidah limehusika na mashambulizi mengi ndani ya Somalia na katika nchi jirani tokea mwaka 2007.