Wananchi wa Kenya waandamana kulaani ukatili wa polisi ya nchi hiyo
Wananchi wa Kenya wamefanya maandamano katika mji mkuu Nairobi, kulaani ukandamizaji na ukatili wa polisi ya nchi hiyo dhidi ya raia.
Kadhalika waandamanaji hao wametaka sheria ifuate mkondo wake kwa kuwawajibisha wahusika wa ukatili huo wa polisi dhidi ya raia. Baadhi ya mabango yaliyokuwa yamebebwa na waandamanaji hao yalikuwa na jumbe zisemazo: Maisha yetu haya thamani; Okoa mustakabali wetu na komesha ukatili wa polisi.
Akthari ya walioshiriki maandamano hayo ni vijana kutoka mitaa ya mabanda jijiji hapo na akina mama ambao vijana wao hususan wa kiume wamekuwa wahanga wa ukatili wa polisi nchini humo katika miaka ya hivi karibuni.

Maandamano haya yanajiri siku chache baada ya Mamlaka Huru ya Kutathmini Mienendo ya Polisi nchini humo (IPOA) kusema kuwa askari polisi wa nchi hiyo wamehusika na mauaji ya raia 15 tangu kuanza kutekelezwa agizo la kutotoka nje nyakati za usiku kwa ajili ya kudhibiti maambukizi ya corona mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu.
Hii ni katika hali ambayo, mnamo Juni 2, mji mkuu wa Kenya ulishuhidia maandamano mengine ya kulaani ubaguzi wa rangi na mauaji ya George Floyd, raia wa Marekani mwenye asili ya Afrika aliyeuliwa kikatili na polisi mmoja mzungu katika mji wa Minneapolis, katika jimbo la Minnesota nchini Marekani.