'Ugonjwa usiojulikana' waua makumi Darfur, Sudan
Maafisa wa afya nchini Sudan wameeleza wasiwasi mkubwa walionao kutokana na ongezeko la vifo 'visivyo vya kawaida' katika kambi za wakimbizi katika eneo la Darfur.
Maafisa hao wamesema idadi ya watu wanaofariki dunia kutokana na 'ugonjwa usijulikana' hususan wazee wenye umri wa maiaka 60 na zaidi katika kambi hizo ni ya kutisha.
Madaktari katika mji wa El Fasher, makao makuu ya mkoa wa Darfur Kaskazini wanasema wanaoaga dunia wana dalili zinazofanana na za ugonjwa wa Covid-19. Wanasema akthari ya walioaga dunia hivi karibuni walikuwa na matatizo ya kupumua, joto kali mwilini na kupoteza hisia ya ladha.
Wafanyakazi wa mashirika ya kibinadamu wanaamini kuwa, virusi vya corona vinasambaa kwa kasi kubwa katika maeneo duni na yaliyotengwa kimaendeleo nchini Sudan hususan katika eneo la Darfur.
Mohamed Hassan Adam, Mkurugenzi wa kambi ya wakimbizi wa ndani ya Abushouk, huko Darfur Kaskazini amesema, "kambi hii imeshuhudia vifo 64 vya kutatanisha ndani ya mwezi mmoja uliopita. Wanaoishi makambini wanakosa hewa, hawawezi kupumua."

Serikali ya Sudan imetangaza marufuku ya kutoka nje katika baadhi ya miji na maeneo ya nchi hiyo kama sehemu ya vita vya nchi nzima vya kupambana na ugonjwa wa COVID-19.
Hadi jana Ijumaa idadi ya watu waliokuwa wamekumbwa na ugonjwa wa corona nchini Sudan ilikuwa imeshafikia 6,879, ambapo 433 kati yao walikuwa wameshafariki dunia. Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Sudan, kesi 193 za corona na vifo 54 vya maradhi hayo vimeripotiwa katika eneo la Darfur pekee.