Rais wa Tanzania: Shule zote zifunguliwe Juni 29, aruhusu harusi
-
John Magufuli
RAIS wa Tanzania, John Pombe Magufuli ameagiza shule zote nchini humo zifunguliwe tarehe 29 Juni 2020 baada ya kuwepo kwa mwenendo mzuri wa maambukizi machache ya ugonjwa wa Corona.
Rais Magufuli ametoa maagizo hayo leo Jumanne tarehe 16 Juni 2020 wakati akihutubia Bunge jijini Dodoma na kusema, hali ya maambukizi ya ugonjwa wa vurusi vya corona (Covid-19) yamepungua hivyo shunguli zingine nazo zirejee kama kawaida;
“Kuanzia Juni 29, 2020, ninatangaza shule zote zifunguliwe, pia shughuli zote ambazo tulizizuia, watu kufunga ndoa, tumewachelewesha watu kuoana wakati huu, ninaruhusu sherehe za ndoa (harusi) ziendelee na shughuli nyingine. Maisha lazima yarudi kama ilivyokuwa zamani, ila nawasihi kuendelea kuchukua tahadhari ya corona.
Shule hizo zilifungwa tangu tarehe Machi 17, 2020 huku shughuli zote zinazohusisha mikusanyiko nazo zilizuiwa ili kuepuka maambukizo ya corona.
Jana Jumatatu tarehe 15 Juni 2020, Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa alihitimisha mkutano wa 19 wa Bunge hilo la 11 na kusema maambukizi ya COVID-19 yamepunguza na wagonjwa waliopo ni 66 pekee.