Jun 20, 2020 07:26 UTC
  • Jeshi la Nigeria lashambulia ngome muhimu ya Boko Haram, laua kadhaa

Kituo cha Kamandi ya kuendeshea operesheni za kundi la kigaidi la Boko Haram kimeharibiwa na kusambaratishwa kikamilifu katika mashambulizi kadhaa ya anga yaliyofanywa na jeshi la Nigeria, huko kaskazini mwa nchi.

Hayo yalisemwa jana Ijumaa na John Enenche, msemaji wa Jeshi la Nigeria ambaye ameongeza kuwa, kituo hicho muhimu cha Boko Haram kilichoharibiwa kiko katika eneo la Yuwe, sehemu ya msitu wa Sambisa, katika jimbo la kaskazini la Borno.

Msitu wa Sambisa uliko kaskazin mashariki mwa Nigeria ni ngome kuu na kituo cha kutoa mafunzo cha kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram.

Bila kutaja idadi, Enenche amesema magadi kadhaa wa Boko Haram wameangamizwa katika operesheni hiyo ya anga ya Jumatano.

Wanachama wa Boko Haram wanaotekeleza hujuma za kutisha Magharibi mwa Afrika

Haya yanajiri siku chache baada ya raia zaidi ya 40 na wanajeshi wasiopungua 20 kuuawa katika mashambulizi mawili tofauti huko kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Mashambulizi hayo yalijiri katika maeneo ya Monguno na Nganzai katika jimbo hilo la Borno. Hakuna kundi lililotangaza kuhusina na ukatili huo, ingawaje wanachama wa Boko Haram wamekuwa wakitekeleza jinai za namna hiyo za umwagaji damu huko kaskazini mwa Nigeria tokea mwaka 2009.

Tags