Watu watano wauawa katika hujuma za kigaidi Somalia
(last modified Sun, 05 Jul 2020 03:49:52 GMT )
Jul 05, 2020 03:49 UTC
  • Watu watano wauawa katika hujuma za kigaidi Somalia

Watu wasiopungua watano wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa kufuatia hujuma za kigaidi nchini Somalia jana Jumamosi.

Katika hujuma ya kwanza mapema Jumamosi, bomu lililipuka katika kituo cha kukusanya kodi katika eneo la Hamar Jajab mjini  Mogadishu.

Taarifa zinasema hujuma hiyo ilitekelezwa na gaidi ambaye aliendesha gari lake lililosheheni bomu kuelekea katika kituo cha polisi cha upekuzi barabrani. Imedokezwa awali gaidi huyo aliwafyatulia risasi polisi ambao nao walijibu kwa kummiminia risasi na hapo gari lake likalipuka. Watu saba wanaripoti kuuawa katika hujuma hiyo akiwemo afisa wa polisi huku gaidi aliyehusika akiangamia papo hapo.

Kwingineko huko Baidoa, mji mkuu wa eneo la kusini maghairbi la Bay, bomu la kutegwa ardhini lililipuka karibu na mghawa ulio nje ya mji huo na kupelekea watu watano kupoteza maisha na wengine 10 kujeruhiwa. Hakuna kundi lolote lililotangaza kuhusika na hujuma hizo lakini kundi la kigaidi la Al Shabab, linalofungamana na mtandao wa Al Qaeda hutekeleza mashambulizi kama hayo mara kwa mara nchini Somalia.

Askari wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika nchini Somalia

Somalia ilitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe karibu miaka 30 iliyopita na magaidi wakufurishaji wa Al Shabab walianzisha hujuma dhidi ya nchi hiyo mwaka 2008.

Mwaka 2011 magaidi wa Al Shabab walifurushwa Mogadishu katika oparesheni ya pamoja ya Jeshi la Somalia na Askari wa Kulinda Amani wa Umoja wa Afrika lakini pamoja na hayo magaidi hao bado wanadhibiti maeneo mengi nchini Somalia.