Jul 06, 2020 03:29 UTC
  • Jeshi la Nigeria liliua wanachama 75 wa Boko Haram mwezi Juni

Jeshi la Nigeria limetangaza habari ya kuuawa wanachama 75 wa kundi la kigaidi la Boko Haram katika operesheni 17 zilizofanyika baina ya Juni Mosi na Juni 30 mwaka huu.

Hayo yalisemwa jana Jumapili na Msemaji wa Jeshi la Nigeria, John Enenche ambaye ameongeza kuwa, magaidi hao wameangamizwa katika operesheni ya Lafiya Dole iliyolenga maficho ya magaidi hao kaskazini mashariki mwa nchi hiyo. 

Ameeleza bayana kuwa, jeshi hilo limefanikiwa pia kuwaokoa mateka 35 waliokuwa mikononi mwa magaidi hao, mbali na kuwatia nguvuni wanachama wanne wa genge hilo la ukufurishaji, wakiwemo wanawake wawili.

Enenche amesema miongoni mwa mateka walionusuriwa katika operesheni hizo ni wanawake 18 na watoto wadogo 16. Msemaji wa Jeshi la Nigeria ameongeza kuwa, askari mmoja wa serikali aliuawa na mwingine kujeruhiwa katika operesheni hizo za mwezi uliopita.

Boko Haram ilianzisha shughuli zake za kigaidi mwaka 2009 kaskazini mwa Nigeria na imepanua wigo wake hadi katika nchi za Niger, Cameroon na kaskazini mwa Chad

Kwa muongo mzima sasa, eneo la kaskazini mashariki mwa Nigeria limekuwa uwanja wa mashambulizi ya magaidi wa Boko Haram ambao mwaka 2014 waliteka nyara mamia ya wasichana katika shule moja ya sekondari mjini Chibok.

Zaidi ya watu elfu 30 wameuawa na wengine wanaokaribia milioni tatu wamelazimishwa kuwa wakimbizi kutokana na mashambulizi ya kundi la Boko Haram nchini Nigeria tokea mwaka 2009.

Tags