Rais wa Kenya atangaza kurefusha muda wa kafyu kukabiliana na Covid-19
Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya leo Jumatatu amerefusha kipindi cha kafyu nchini humo kwa siku nyingine 30 na kupiga marufuku uuzaji wa pombe migahawani ili kuzuia maambukizi ya COVID-19 nchini humo.
Hadi kufikia sasa Kenya imeripoti kesi 17,603 za maambukizi ya corona na vifo 280. Wizara ya Afya ya Kenya jana Jumapili ilitangaza kuwa kesi nyingine 960 za maambukizi zimethibitishwa nchini, kiwango ambacho ni cha juu zaidi kusajiliwa kwa siku moja tangu kuripotiwe kesi ya kwanza ya maambukizi ya corona nchini humo mwezi Machi mwaka huu.
Akihutubia taifa kwa njia ya televisheni, Rais Kenyatta amesema kuwa ukweli mchungu ni kwamba, Kenya inapigana vita na adui asiyeonekana.

Nchi hiyo ya mashariki mwa Afrika ilikuwa na kesi za corona karibu 7,900 na vifo 160 wakati Rais Uhuru Kenyatta alipohutubia taifa kwa njia ya televisheni mnano Julai 6 mwaka huu.
Ripoti zinasema kuwa maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19 au corona barani Afrika pia yanaongezeka kwa kasi na hadi kufikia Jumapili wiki hii jumla ya watu 828,214 walikuwa tayari wamepatwa na maambukizi ya virusi hivyo barani humo.
Kwa mujibu wa Kituo cha Kudhibiti Magonjwa Barani Africa (Africa-CDC) hadi sasa walioaga dunia kutokana na COVID-19 barani Afrika ni 17,509 katika nchi 54 barani humo.