Aug 11, 2020 11:23 UTC
  • Wapiganaji wa Janjaveed wa Sudan wapelekwa Libya kujiunga na Haftar

Jeshi la Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa nchini Libya limetangaza kuwa mfasara uliokuwa na magari 70 ya kijeshi yakibeba silaha na mamluki wa kundi la Janjaweed umevuka maeneo maarufu kama Hilali ya Mafuta ya Libya ukiuelekea katika mji wa Sirte kwa ajili ya kumsaidia jenerali muasi, Khalifa Haftar.

Habari hiyo imetangazwa baada ya Shirika la Mafuta la Taifa nchini Libya kutahadharisha kwamba, kuna uwezekano wa kutokea mlipuko mkubwa kama ule wa bandari ya Beirut kutokana na mrundikano mkubwa wa wanajeshi na zana za kivita katika bandari na visima vya mafuta nchini Libya na uwepo wa mada za ammonium nitrate katika maeneo hayo.

Mkuu wa shirika hilo ametahadharisha kwamba, kuna uwezekano wa kutokea mlipuko mkubwa katika bandari za mafuta za Libya kutokana na tani 25 za mada za ammonium nitrate zilizoko katika maeneo hayo na amesisitiza udharura wa maeneo hayo kutenganishwa kikamilifu na medani za vita ili kuepusha maafa makubwa kwa raia wa kawaida.

Wapiganaji wa Janjaweed kutoka Sudan wanapelekwa Libya kujiunga na jenerali Haftar

Mustafa Sanalla ametahadharisha kuwa ongezeko la makundi ya kijeshi na kuwepo kwa vifaru na maghala mengi yaliyojaa mafuta katika bandari za mafuta za Libya vinazidisha hatari ya kutokea maafa makubwa.

Sanalla ameongeza kuwa, bandari za mafuta za nchi hiyo zimefungwa na uuzaji nje bidhaa hiyo umesimamishwa, na iwapo maghala yaliyojaa mafuta yanapatwa na cheche au kitu chochote chenye moto kutashuhudiwa maafa makubwa zaidi ya yale ya bandari ya Beirut.

Mlipuko mkubwa uliotokea jioni ya Jumanne iliyopita katika bandari ya Beirut umesababisha vifo vya watu wasiopungua 163. Watu wengine zaidi ya elfu tano wamejeruhiwa.

Tags