Tanzania yatangaza vita dhidi ya uharibifu wa mazingira
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i6280-tanzania_yatangaza_vita_dhidi_ya_uharibifu_wa_mazingira
Serikali nchini Tanzania imesema kuwa, hali ya mazingira ya nchi hiyo ni mbaya kutokana na kukithiri kwa uharibifu mkubwa wa mazingira, ambapo kwa sasa takribani asilimia 61 ya ardhi yake iko kwenye hatarini ya kuwa jangwa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 02, 2016 23:53 UTC
  • Tanzania yatangaza vita dhidi ya uharibifu wa mazingira

Serikali nchini Tanzania imesema kuwa, hali ya mazingira ya nchi hiyo ni mbaya kutokana na kukithiri kwa uharibifu mkubwa wa mazingira, ambapo kwa sasa takribani asilimia 61 ya ardhi yake iko kwenye hatarini ya kuwa jangwa.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira na Muungano, January Makamba na kuongeza kuwa, kutokana na hali hiyo, serikali ya nchi hiyo imeamua kutangaza vita dhidi ya uharibifu huo wa mazingira, ikiwa ni pamoja na kuainisha mikakati yenye lengo la kutengeneza Tanzania ya kijani. Katika hali hiyo, serikali imetangaza kampeni ya kitaifa ya upandaji miti nchi nzima, ikiwa ni pamoja na kuanza mchakato wa kubuni sheria ya kudhibiti uharibifu huo, kukiwemo pia kusimamia utaratibu wa upandaji miti kuanzia ngazi ya vijiji, kata, vitongoji, tarafa, wilaya na mikoa. Akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2016/17, Makamba amesema kila mwaka nchi hiyo inapoteza hekta 372,000 sawa na ekari milioni moja za misitu. Amesema hali hiyo inatokana na matumizi makubwa ya bidhaa za misitu, akieleza kuwa asilimia 90 ya nishati inayotumika nchini inatokana na misitu na kwa Jiji la Dar es Salaam pekee hutumia magunia 200,000 hadi 300,000 ya mkaa kwa mwezi. Itafahamika kuwa, Tanzania ni miongoni mwa nchi za Kiafrika zinazotajwa kuwa na asilimia kubwa ya uharibifu wa mazingira katika eneo la mashariki mwa bara hilo.