Gaidi ajiripua mbele ya msikiti, kusini mwa Somalia
Duru za habari za ndani na nje ya Somalia zimetangaza kuwa gaidi mmoja amejiripua kwa mabomu nje ya msikiti mmoja wa kusini mwa nchi hiyo.
Miongoni mwa vyombo vya habari vilivyoripoti habari hiyo ni shirika la habari la Anadolu la nchini Uturuki ambalo limesema kuwa, gaidi mmoja aliyekuwa amejifunga mabomu amejiripua nje ya msikiti mmoja katika mji wa Kismayo wa kusini mwa Somalia na kuua kwa uchache Waislamu wawili na kujeruhi wengine 12.
Vyombo vya habari vya ndani ya Somalia navyo vimeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, viongozi kadhaa wa kieneo, akiwemo mkuu wa kitengo cha biashara cha eneo lenye utawala wa ndani la Jubaland ni miongoni mwa watu waliojeruhiwa kwenye mripuko huo, na hadi tunapokea habari hii, hali yake ilikuwa mahututi.
Kwa kawaida genge la kigaidi na la ukufurishaji la al Shabab ndilo linalohusika na mashambulio ya aina hiyo hata kama baadhi ya wakati halitangazi kuhusika.
Genge hilo lililojitangaza kuwa ni sehemu ya mtandao wa kigaidi wa al Qaida, hadi hivi sasa limeshatangaza mara chungu nzima kuhusika na mashambulizi ya kigaidi ya ndani ya nje ya Somalia.
Tangu mwaka 2007 hadi hivi sasa, genge hilo linaendesha mashambulizi ya kigaidi na ya kujiripua kwa mabomu kwa madai ya kutaka kuipindua serikali kuu ya Somalia.
Mwaka 2011 jeshi la Somalia kwa kushirikiana na wanajeshi wa Umoja wa Afrika, lilifurusha genge hilo katika miji yote mikubwa ukiwemo Mogadishu. Hata hivyo bado genge la al Shabab linadhibiti baadhi ya maeneo ya vijijini na mashambani huko Somalia.