Hasara za mafuriko zaongezeka nchini Sudan
(last modified Sat, 19 Sep 2020 07:32:48 GMT )
Sep 19, 2020 07:32 UTC
  • Hasara za mafuriko zaongezeka nchini Sudan

Idara ya Ulinzi wa Raia nchini Sudan imetangaza habari ya kuongezeka hasara za roho za watu na mali kutokana na mafuriko yaliyoikumba nchi hiyo. Kwa mujibu wa idara hiyo, zaidi ya watu laki saba na 70 elfu wamepata hasara kutokana na mafutiko hayo.

Televisheni ya RT imemnukuu Abdul Jalil Abur Rahim, Msemaji wa Baraza la Ulinzi wa Taifa wa Raia nchni Sudan akisema jana Ijumaa kwamba maeneo yaliyopata hasara kutokana na mafuriko hayo ni mengi, mashamba na ardhi za kilimo zimeharibiwa huku wafanyakazi wa masuala ya misaada wakiendelea na juhudi zao za kupunguza kadiri wanavyoweza kiwango cha hasara hizo kwa kutumia suhula walizo nazo.

Wiki iliyopita, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) ilitangaza kuwa zaidi ya watu nusu milioni wa Sudan wameathiriwa na mafuriko makubwa yaliyotokea nchini humo kutokana na mvua kali zilizosababisha kujaa maji ya Mto Nile.

Mafuriko yanaendelea kusababisha hasara nchini Sudan

 

Taarifa iliyotolewa na OCHA ilisema kuwa, hadi Jumanne ya wiki iliyopita zaidi ya watu laki tano na 57 elfu walikuwa wamedhuriwa na mafuriko nchini Sudan na kwamba maeneo ya Khartoum, kaskazini mwa Darfur na Sinar ndiyo yaliyopata hasara kubwa zaidi kutokana na mafuriko hayo. Taarifa hiyo iliongeza kuwa, mvua kali zinazoendelea kunyesha nchini Sudan zinatishia kuzuka maradhi ya kuambukiza na kukwamisha juhudi za kudhibiti maambukizi  ya kirusi cha corona. 

Sasa hivi Idara ya Ulinzi wa Rais nchini humo inasema idadi ya waathirika wa mafuriko hayo imepindukia laki saba na 70 elfu. Siku chache zilizo, watu 121 wameripotiwa kuongezeka katika idadi ya waliofariki dunia kutokana na mafuriko hayo. 

Tags