Jeshi la Somalia laua wanamgambo 16 wa al-Shabaab
Wanachama 16 wa kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab wameangamizwa katika operesheni ya jeshi la Somalia katika jimbo la Galmadug, katikati mwa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
Mashuhuda wanasema magaidi hao wa al-Shabaab wameuawa katika makabiliano baina yao na wanajeshi wa Somalia katika mji wa Bula'ale ulioko katika eneo la Galgadud, jimboni Galmadug.
Habari zaidi zinasema kuwa, silaha kadhaa zilizokuwa mikononi mwa wanamgambo hao zimenaswa na maafisa usalama katika operesheni hiyo ya Jumatatu.
Inaarifiwa kuwa, makabiliano makali ya risasi yalishuhudiwa jana katika mji wa Dhusamareb, makao makuu ya kiutawala ya jimbo la Galmadug.
Wanachama kadhaa wa genge hilo la ukufurishaji lenye mfungamano na mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda wametiwa mbaroni katika operesheni hiyo, na wanatazamiwa kupandishwa kizimbani katika wiki chache zijazo.
Haya yanajiri chini ya wiki moja baada ya wapiganaji wengine saba wa al-Shabaab kuuawa kwenye mapambano makali na jeshi la Somalia katika mji wa Awdhigle mkoani Lower Shabelle, kusini mwa Somalia.
Vikosi vya serikali ya Somalia hivi karibuni vimeimarisha operesheni dhidi ya genge la al-Shabaab kwenye maeneo ya katikati na kusini mwa nchi hiyo.