Oct 01, 2020 07:54 UTC
  • Watoto 144 waaga dunia kwa utapiamlo nchini Angola

Watoto 144 wamepoteza maisha kutokana na utapiamlo katika kipindi cha miezi sita ya kwanza ya mwaka huu katika mkoa wa Bié katikati mwa Angola.

Ripoti ya wataalamu wa afya nchini humo inasema, vifo hivyo ni miongoni mwa kesi mpya 1,939 zilizoripotiwa za watoto wanaosumbuliwa na utapiamlo katika nchi hiyo yenye utajiri wa mafuta.

Edna Mendonça, Mkuu wa Mpango wa Lishe katika mkoa huo amesema miongoni mwa mambo yaliyochangia kuongezeka utapiamlo miongoni mwa watoto nchini humo ni uhaba wa chakula katika baadhi ya familia, na pia baadhi ya watoto hao kusumbuliwa kwa muda mrefu na magonjwa kama malaria, kifua kikuu, kuendesha, upungufu wa damu mwilini (anaemia) na HIV/Ukimwi.

Aghalabu ya mikoa ya nchi hiyo imekuwa ikitegemea misaada na bidhaa za kukabiliana na utapiamlo kutoka Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (Unicef).

Mbali na mafuta, Angola pia ina utajiri wa madini hasa almasi

Licha ya kuwa Angola ni nchi ya pili kwa uuzaji nje mafuta barani Afrika, lakini ufisadi na ubadhirifu wa mali za umma umewasababishia wananchi wa nchi hiyo masaibu mengi.

Mishoni mwa mwaka jana, Waziri wa Sheria wa Angola alisema kuwa, mwaka huo 2019 nchi hiyo ilikamata zaidi ya dola bilioni tano zilizokuwa zimeibiwa kwenye mifuko ya taifa ya ndani na nje ya nchi.

Tags