Tume ya Uchaguzi Tanzania yamfungia Lissu kufanya kampeni
Kamati ya Maadili ya Kitaifa ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania (NEC) imemsimamisha mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, kufanya kampeni kwa muda wa siku saba, kwa madai ya kukiuka kanuni na taratibu za uchaguzi.
Taarifa iliyotolewa leo Ijumaa na kutiwa saini na Katibu wa Kamati ya Maadili ya Tume ya Uchaguzi ya NEC, Emmanuel Kawishe imesema kamati yake imeafikiana kumsimamisha Tundu Lissu kufanya kampeni za uchaguzi kwa siku saba, kwa kukiuka maadili ya uchaguzi na kutoa lugha ya kichochezi na tuhuma zisizothibitika kinyume cha kanuni ya 2.1 (a), (b), (d) na (n).
Taarifa hiyo imesema Lissu haruhusiwi kufanya kampeni hadi Oktoba 9 wakati adhabu hiyo itakapomalizika, lakini ana haki ya kukata rufaa kwenye Kamati ya Rufaa ya NEC kupinga uamuzi huo.
Wakati huo huo Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam leo Ijumaa limesitisha wito wa kumtaka Lissu kufika kituo cha polisi na badala yake kuendelea na ratiba za kampeni za uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, hivi karibuni Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch (HRW) lilitangaza kuwa, mamlaka nchini Tanzania imeongeza hatua za ukandamizaji dhidi ya vyama vya upinzani na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu.
Uchaguzi mkuu nchini Tanzania umepangwa kufanyika tarehe 28 ya mwezi huu wa Oktoba huku mchuano mkali katika kinyang'anyiro cha urais katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ukitazamiwa kuwa baina ya Tundu Lissu wa CHADEMA na Rais John Magufuli anayewania muhula wa pili kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).