Wanajeshi 13 wa Somalia wauawa katika makabiliano na al-Shabaab
(last modified Fri, 16 Oct 2020 03:10:58 GMT )
Oct 16, 2020 03:10 UTC
  • Wanajeshi 13 wa Somalia wauawa katika makabiliano na al-Shabaab

Kwa akali askari 13 wa Jeshi la Taifa la Somalia wameuawa katika makabiliano makali baina yao na wanamgambo wa kundi la kigaidi la al-Shabaab karibu na wilaya ya Afgoye, kaskazini magharibi mwa mji mkuu, Mogadishu.

Meja Mohamed Ali, afisa wa ngazi za juu wa jeshi la Somalia ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, wanamgambo hao walitekeleza shambulizi hilo hapo jana kwa lengo la kulipiza kisasi cha kuuawa wanachama wenzao.

Amesema siku ya Jumatano wanajeshi wa Somalia walivamia maficho ya al-Shabaab katika msitu na vichaka vilivyoko karibu na wilaya ya Afgoye, yapata kilomita 30 kutoka Mogadishu, na kufanikiwa kuangamiza wanne miongoni mwao, na ndiposa wenzao wakafanya hujuma ya ulipizaji kisasi hiyo jana.

Katika hali ambayo jeshi la Somalia linasisitiza kuwa idadi ya askari wake waliouawa ni 13, lakini kundi hilo la kigaidi kupitia msemaji wake, Abdiasis Abu Musab linadai kuwa limeua wanajeshi 24.

Maafisa usalama karibu na msitu ambapo wanajificha al-Shabaab

Haya yanajiri chini ya wiki moja baada ya wanachama watano wa kundi hilo la kigaidi kuangamizwa katika operesheni ya jeshi la Somalia katika mji wa Dinsor, eneo la Bay kusini mwa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika. Aidha mapema mwezi huu, magaidi wasiopungua wanane waliuliwa katika operesheni ya mashambulio iliyofanywa na jeshi la Somalia kaskazini magharibi mwa mji mkuu wa nchi hiyo Mogadishu.

Tangu mwaka 2007 kundi la kigaidi la al-Shaabab limekuwa likifanya operesheni za hujuma na mashambulio kwa lengo la kuiangusha serikali ya Somalia.

Tags