Magaidi 17 wa al-Shabaab wauawa na jeshi la Somalia, Hiran
Jeshi la Taifa la Somalia SNA limetangaza habari ya kuwaangamiza wanachama 17 wa kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab katika eneo la Hiran, katikati mwa nchi hiyo.
Hayo yalitangazwa jana Alkhamisi na Ahmed Mohamed, Kamanda wa Kikosi cha 27 cha Jeshi la Taifa la Somalia na kuongeza kuwa, magaidi hao wameuawa katika operesheni ya Jumatano ya vikosi vya jeshi katika mji wa Bule Burde.
Amesema miongoni mwa waliouawa katika operesheni hiyo ni kamanda anayesimamia operesheni za al-Shabaab katika mji wa Bule Burde, Abdulkadir Fidow na makamanda wengine wawili.
Jumanne iliyopita pia, wanajeshi wa Somalia waliwaua magaidi 11 wa kundi la al-Shabaab akiwemo kamanda mwandamizi katika mji wa Sablale mkoa wa Lower Shabelle.
Tangu mwaka 2007, kundi la kigaidi la al-Shabaab lenye mfungamano na mtandao wa al Qaida limekuwa likifanya mashambulizi ndani ya Somalia kwa lengo la kuiangusha serikali kuu ya nchi hiyo inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika.
Jeshi la Somalia kwa kusaidiwa na kikosi maalumu cha Umoja wa Afrika AMISOM lilifanikiwa kuwafurusha magaidi wa al Shabab katika mji mkuu Mogadishu, mwezi Agosti 2011.
Hata hivyo bado wanamgambo hao wanadhibiti maeneo ya vijijini ya kusini na katikati mwa Somalia na wanafanya mashambulizi ya mara kwa mara ya kuvizia katika mji mkuu Mogadishu na maeneo mengine.