Jeshi la Somalia lawaangamiza mamluki wenye mfungamano na kundi la al Shabaab
(last modified Tue, 01 Dec 2020 08:00:50 GMT )
Dec 01, 2020 08:00 UTC
  • Jeshi la Somalia lawaangamiza mamluki wenye mfungamano na kundi la al Shabaab

Mamluki kadhaa wenye mfungamano na kundi la kigaidi la al Shabaab la huko Somalia wameuawa katika mapigano kati ya kundi hilo na jeshi la Somalia.

Jeshi la Somalia jana Jumatatu lilitangaza kuwa  limewaua mamluki 20 wa al Shabaab katika shambulio liliofanywa na kundi hilo kwenye kambi ya jeshi katika kitongoji cha Baadwin katikati mwa Somalia.  

Redio ya jeshi la Somalia imetangaza kuwa askari jeshi wa nchi hiyo kwa kushirikiana na wenyeji wa eneo hilo wamefanikiwa kutoa pigo kwa magaidi hao. Mbali na kuwaangamiza wanamgambo wa al Shabaab katika mapigano hayo, jeshi la Somalia limekamata ngawira na pia makamanda wawili wa kundi hilo.  

Redio ya jeshi la Somalia hata hivyo haikuashiria idadi ya wanajeshi wa Somalia waliouawa katika mapigano hayo. Awali kundi la al Shabaab lilitangaza kuwa limeidhibiti kambi moja ya jeshi na magari matano ya deraya.

Kundi la kigaidi la al Shabaab ambalo linafuata fikra na mielekeo ya kufurutu ada ya mtandao wa kigaidi wa al Qaida lilitangaza uwepo wake huko Somalia mwanzoni mwa mwaka 2004. Jeshi la Somalia kwa kuungwa mkono na Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika katika miaka ya karibuni limefanikiwa kuendesha mapambano dhidi ya al Shabaab. 

Wanajeshi wa Umoja wa Afrika katika vita dhidi ya al Shabaab 

 

Tags