Dec 25, 2020 13:39 UTC
  • Boko Haram yashambulia vijiji kadhaa na kuua katika mkesha wa Krismasi

Watu saba wameuawa huku wengine wengi wakijeruhiwa baada ya kundi la kigaidi la Boko Haram kushambulia vijiji kadhaa katika majimbo ya Borno na Adamawa nchini Nigeria, usiku wa kuamkia leo.

Duru za habari zimeliambia shirika la habari la AFP kuwa, wanamgambo wa genge hilo hapo jana walishambulia kijiji cha Pemi katika jimbo la Borno, kaskazini mashariki mwa nchi.

Mashuhuda wanasema magaidi hao waliokuwa juu ya pikipiki na malori walishambulia kijiji hicho na kuanza kufyatua risasi ovyo, mbali na kuchoma moto nyumba za wakazi wa kijiji hicho.  Kadhalika wanachama hao wa Boko Haram wameiba chakula cha msaada walichopewa wakazi wa kijiji hicho kwa ajili ya sherehe za Krismasi zilizoadhimishwa leo.

Ayuba Alamson, kiongozi wa kijamii katika kijiji cha Pemi jimboni Borno amesema maiti moja imepatikana mapema leo na kupelekea idadi ya wanakijiji waliouawa katika shambulio hilo la jana usiku kufikia saba.

Jimbo la Borno la kaskazini mashariki mwa Nigeria

Habari zaidi zinasema kuwa, magaidi hao pia wamechoma moto hospitali, kanisa, na kumteka nyara kasisi mmoja katika kijiji hicho kabla ya kutorokea katika msitu wa Sambisa.

Wakati huo huo, wabeba silaha wanaosadikiwa kuwa wanachama wa Boko Haram hapo jana walivamia kijiji cha Garkida katika jimbo la Adamawa na kufanya wizi mkubwa katika maduka ya dawa na chakula kabla ya kuchoma moto nyumba za wakazi wa kijiji hicho.

Idadi ya waliouawa au kujeruhiwa katika shambulio hilo la Adamawa haijajulikana kufikia sasa.

 

Tags