Uganda yakanusha madai kuwa jeshi lake limeua magaidi 189 wa al-Shabaab
Serikali ya Uganda imekadhibisha taarifa kuwa jeshi la nchi hiyo UPDF limeua wanachama 189 wa genge la al-Shabaab kusini magharibi mwa mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.
Adonia Ayebare, Mwakilishi wa Kudumu wa Uganda katika Umoja wa Mataifa mjini New York amesema madai hayo ya kuuawa wanachama 189 wa al-Shabaab katika shambulizi la kushtukiza la UPDF Ijumaa iliyopita nchini Somalia ni ya uwongo na hayana ukweli wowote.
Ameutaka uma upuuzilie mbali habari hizo zilizochapishwa na kurushwa hewani na vyombo mbalimbali vya habari. Mwanadiplomasia huyo wa ngazi za juu wa Uganda amesema binafsi amezungumza na viongozi wa UPDF ambao wamesisitiza kuwa habari hizo ni feki.
Ijumaa iliyopita, shirika la habari la Reuters lilinukuu kile kilichotajwa kuwa taarifa kutoka duru za ndani ya jeshi la Uganda UPDF ikisema kuwa, askari wa nchi hiyo wanaolinda amani huko Somalia chini ya mwavuli wa kikosi cha Umoja wa Afrika AMISOM wamevamia maficho ya genge hilo la kigaidi katika kijiji cha Sigaale, yapata kilomita 99 magharibi mwa mji mkuu Mogadishu na kuua wanamgambo 189 wa genge hilo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wanajeshi wa Uganda walikamata pia silaha pamoja na makamanda wawili wa genge hilo la kigaidi; mbali na kusambaratisha pia mkutano wa genge hilo la ukufurishaji na kujeruhi magaidi kadhaa katika eneo la Doncadaafeedow lililoko umbali wa kilomita 7 kutoka mji wa Janaale.
Wanajeshi 4,500 wa Uganda wako nchini Somalia tokea mwaka 2007, chini ya mwavuli wa kikosi cha Umoja wa Afrika maarufu kwa jina la AMISOM.