Kuakhirishwa kesi ya Sheikh Ibrahim Zakzaky nchini Nigeria
Katika hali ambayo Waislamu nchini Nigeria wameshiriki katika maandamano ya amani ya kutaka kuachiliwa huru Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria, mwendesha mashtaka mkuu nchini humo ameakhirisha tena kesi ya kiongozi huyo wa harakati ya Kiislamu.
Kwa mujibu wa mwendesha mashtaka mkuu wa Nigeria, kesi ya Sheikh Zakzaky sasa itasikilizwa Machi 10.
Sheikh Ibrahim Zakzaky na mke wake, Malama Zeenat walikamatwa mnamo Disemba 13 mwaka 2015 wakati wanajeshi walipohujumu ukumbi wa kidini ujulikanao kama Husseiniya ya Baqiyatullah katika mji wa Zaria jimboni Kano kaskazini mashariki mwa nchi hiyo. Wawili hao wamekuwa wakishikiliwa tokea wakati huo ambapo hali ya kiafya ya Sheikh Zakzaky ni mbaya sana na ofisi ya kiongozi huyo wa harakati ya Kiislamu imekuwa ikitoa taarifa mara kwa mara kuhusu kuendelea kuzorota afya yake.
Halikadhalika katika miezi ya hivi karibuni kufuatia kuibuka kirusi cha corona au COVID-19, hali ya kiafya ya Sheikh Zakzaky na mke wake imezidi kuwa mbaya. Siku chache zilizopita, Ofisi ya Allamah Sheikh Ibrahim Zakzaky ilitangaza kuwa, Mahakama Kuu ya Kaduna iliwaamuru wakuu wa gereza katika jimbo wamhamishie hospitalini mke wa Sheikh Zakzaky, Malama Zeenat baada ya kubainika kuwa ameambukizwa corona.
Hali ya Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria nayo pia si nzuri na si tu kuwa wakuu wa Nigeria hawajachukua tahadhari zozote za kuhakikisha haambukizwi COVID-19 bali hata kuna taarifa kuwa mtu mwenye COVID-19 alipelekwa kwa makusudi katika eneo anaposhikiliwa Sheikh Zakzaky jambo ambalo limelalamikiwa vikali na wafungwa.

Katika miaka ya hivi karibuni, serikali ya Nigeria imeshadidisha ukandamizaji wa Waislamu nchini humo. Utawala wa Nigeria umepiga marufuku au kuweka vizingiti katika mijumuiko ya kidini kama ile ya siku za Taasua na Ashura na wanaoshiriki katika mikusanyiko hiyo wamekumbana na mkono wa chuma wa vikosi vya usalama. Ni wazi kuwa serikali ya Nigeria inazitazama harakati za Waislamu kwa jicho la tishio kwa usalama. Kujipenyeza Saudia Arabia na Israel nchini Nigeria kunatajwa kuwa moja ya sababu ambazo zimeipelekea serikali ya nchi hiyo kuwakandamiza Waislamu hasa wafuasi wa Harakati ya Kiislamu. Kwa mtazamo wa wakuu wa Saudia uwepo wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria ambayo imeimarika sana miongo ya hivi karibuni ni tishio katika kueneza itikadi ya Uwahhabi nchini humo. Nao wakuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel wanalenga kupora utajiri mkubwa wa mafuta na vyanzo vingine vya asili katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika na hivyo hawataki harakati yoyote yenye kuleta mwamko miongoni mwa wananchi na hasa Waislamu na ndio maana wameishawishi serikali ya Nigeria izidishe mashinikizo dhidi ya Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu Sheikh Ibrahim Zakzaky.
Lakini pamoja na kuwepo mashinikizo hayo yote, Waislamu wa Nigeria wamekuwa wakiandamana mara kwa amra wakitaka Sheikh Zakzaky aachiliwe huru. Katika maandamano ya hivi karibuni, maafisa wa polisi waliwahujumu Waislamu ambao walikuwa wakiandamana kwa amani kulalamikia namna mahakama inavyoendesha kesi ya Sheikh Zakzaky. Hatua ya hivi karibuni ya serikali ya Nigeria kuakhirisha tena kesi ya Sheikh Zakzaky inaonekana ni mbinu ya wazi kabisa ya kupoteza wakati ili kumuangamiza hatua kwa hatua mwanazuoni huyo wa Kiislamu.

Wakili wa Sheikh Zakzaky, Ishaq Adam anasema kuhusuana na nukta hiyo kuwa: "Marekani, Israel na Saudi Arabia zimempa kazi Rais Muhammadu Buhari na kumataka ahakikishe kuwa kiongozi wa Waislamu wa Kishia Nigeria anauawa. Saudia Arabia imewapa wakuu wa serikali ya Abuja mamilioni ya dola kufanikisha jambo hilo.
Ingawa serikali ya Nigeria inaendeleza jitihada za kummaliza Sheikh Zakzaky, lakini Waislamu nchini humo hawatasita katika jitihada zao za kutaka kiongozi wa Harakati ya Kiislamu aachiliwe. huru. Waislamu wa Nigeria wana azma imara ya kuendelea kupaza sauti ya kutaka Sheikh Zakzaky aachiliwe huru.