Feb 10, 2021 23:34 UTC
  • Makumi wauawa katika hujuma za wabeba silaha Nigeria

Makumi ya watu wameuawa katika mashambulizi kadhaa ya magenge ya wabeba silaha katika wilaya tano za eneo la kaskazini magharibi mwa Nigeria.

Kamishna wa Usalama wa Taifa wa Nigeria, Samuel Aruwan amesema magenge ya watu waliojizatiti kwa silaha yameshambulia wilaya za Birnin Gwari, Giwa, Chikun, Igabi na Kauru huko kaskazini magharibi mwa nchi na kuua watu wasiopungua 23.

Amesema wilaya iliyoathirika zaidi katika hujuma hizo za wabeba silaha ni Birnin Gwari ambapo watu kumi wameuawa.

Haijabainika ni kundi gani limehusika na mashambulizi hayo, ingawaje genge la Boko Haram lenye uhusiano na kundi la kigaidi la ISIS (Daesh) limekuwa likifanya hujuma za namna hiyo katika maeneo ya kaskazini mwa Nigeria.

Wanachama wa Boko Haram

Haya yanajiri siku chache baada ya maafisa usalama 11 wakiwemo wanajeshi wanne kuuawa katika shambulio la bomu la kutegwa ardhini la kundi la kigaidi la Boko Haram katika jimbo hilo la Borno huko kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Makumi ya maelfu ya watu wakiwemo maafisa usalama wameuawa tangu kundi la kigaidi la Boko Haram liliposhika silaha mwaka 2009 huko kaskazini mwa Nigeria, na kuanzia hapo likaanza kueneza jinai na mashambulizi yake huko Niger, Chad na kaskazini mwa Cameroon. 

Tags