Feb 14, 2021 07:55 UTC
  • Mripuko mpya wa Ebola waripotiwa Guinea, watu 4 wapoteza maisha

Watu wanne wameripotiwa kuaga dunia kutokana na ugonjwa wa Ebola katika eneo la Nzerekore, kusini mashariki mwa Guinea.

Hayo yamesemwa na Remy Lamah, Waziri wa Afya wa Guinea ambaye ameongeza kuwa, kuripuka upya maradhi hayo baada ya miaka mitano kumeibua hofu miongoni mwa wananchi wa nchi hiyo, ambao wanaendelea kukabiliana na makali ya janga la Corona.

Amesema mripuko huu ni wa kwanza tokea janga la Ebola lishuhudiwe katika nchi hiyo na nchi jirani baina ya mwaka 2013 na 2016.

Naye Sakoba Keita, Mkuu wa Wakala wa Kitaifa wa Usalama wa Afya wa Guinea amenukuliwa na vyombo vya habari vya nchi hiyo akisema kuwa, mmoja wa watu walioaga dunia katika mripuko huu mpya ni muuguzi ambaye aliambukizwa ugonjwa huo mwishoni mwa Januari na kuaga dunia mapema mwezi huu.

Ameongeza kuwa, miongoni mwa watu waliohudhuria maziko ya muuguzi huyo, wanane miongoni mwao wameonyesha dalili za maradhi hayo kama kuendesha (kuharisha), kutapika na kutokwa na damu.

Chanjo ya Ebola

Haya yanajiri wakati huu ambao Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imethibitisha kesi tatu mpya za ugonjwa huo katika mji wa Butembo jimboni Kivu Kaskazini, eneo ambalo lilikuwa kitovu cha mlipuko wa 10 wa ugonjwa huo uliotangazwa kumalizika mwezi Juni mwaka jana.

Ikumbukwe kuwa, mripuko mkubwa zaidi wa ugonjwa hatari wa Ebola ulitokea baina ya Disemba 2013 na Aprili 2016 na kuua zaidi ya watu 11,000 katika nchi za Guinea, Liberia na Sierra Leone huko magharibi mwa bara la Afrika.

 

Tags