Serikali ya Somalia yaikosoa Imarati kwa kuwaunga mkono wapinzani wa Kisomali
-
Osman Abokor Dube
Serikali ya Somalia imeikosoa Imarati kutokana na kuwaunga mkono wapinzani wa serikali ya Mogadishu.
Waziri wa Habari wa Somalia ambaye alikuwa akijibu taarifa iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Imarati kuhusiana na yanayojiri ndani ya Somalia amesema kuwa, Abu Dhabi imeamua kukanyaga kanuni za kidiplomasia na kuwaunga mkono wapinzani wa Kisomali.
Waziri wa Habari wa Somalia Osman Abokor Dube ameitaka Imarati ieombe radhi kwa kutoa taarifa kama hiyo inayokanyaga mamlaka ya kujitawala ya Somalia.
Dube ameituhumu Imarati kwamba imachochea machafuko nchini Somalia na kuielekeza nchi hiyo katika hali inayofanana na ile ya Yemen au Libya na kwamba inaingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo kupitia harakati zake katika baadhi ya majimbo ya Somalia.
Hivi karibuni Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Imarati ilitoa taarifa kuhusu matukio ya ndani ya Somalia ikikosoa mwenendo wa serikali ya Mogadishu dhidi ya wapinzani wa serikali.
Katika miaka ya karibuni Imarati imekuwa ikifanya jitihada za kupanua ushawishi wake katika nchi za Afrika hususan katika eneo la Pembe ya Afrika kwa kutumia fedha za utajiri wa mafuta.