Sudan: Hakuna ufumbuzi wa kijeshi wa mgogoro wa bwawa la Renaissance
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Sudan amesema kuwa, ni jambo lililo mbali kwamba mgogoro wa bwawa la Renaissance unaweza kutatuliwa kwa njia za kijeshi ili kuizuia Ethiopia kuendeleza mradi ujenzi wa bwawa hilo juu ya maji ya Mto Nile.
Mariam Sadiq al-Mahdi amewaambia waandishi habari akiwa Doha nchini Qatar kwamba, hakuna nafasi yoyote ya ufumbuzi wa kijeshi wa mgogoro wa bwawa la Renaissance na kwamba Khartoum inazungumzia utatuzi wa kisiasa wa mgogoro huo.
Sadiq al Mahdi amesisitiza kuwa, zinafanyika juhudi za kuishirikisha jamii ya kimataifa na zaidi nchi za Kiafrika ili kuizuia Ethiopia kuendeleza ujenzi wa bwawa hilo la kuvuruga amani ya nchi mbili za Misri na Ethiopia.
Matamshi hayo ya Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Sudan yametolewa siku kadhaa baada ya Rais Abdel Fattah al Sisi wa Misri kutishia kwamba "Cairo itatoa jibu lisilotasawarika iwapo nchi yake itapata madhara kutokana na bwana la Renaissance linalojengwa na Ethiopia juu ya maji ya Mto Nile."
Rais wa Misri alisisitiza kuwa maji ya Misri ni mstari mwekundu na anayetaka kujaribu atakiona cha mtemakuni.
Wakati huo Naibu Waziri Mkuu wa Ethiopia amesema leo Ijumaa kwamba, nchi yake ina imani na ufumbuzi wa nchi za Kiafrika katika mazunguzo ya bwawa la Renaissance. Amesema Addis Ababa imeazimia kudumisha mazungumzo ya pande tatu chini ya usimamizi wa Umoja wa Afrika (AU) ili kupata suluhisho la mzozo huo.
Misri na Sudan zinasema ujenzi wa bwawa hilo ambalo limegharimu karibu dola bilioni nne, utapunguza maji ya nchi hizo na hivyo kuvuruga maisha ya mamilioni ya watu. Ethiopia nayo inasisitiza kuwa ujenzi wa bwawa hilo ni muhimu kwa ajili ya kueneza umeme katika nchi hiyo ili kuimarisha sekta ya viwanda na pia kuuza bidhaa hiyo katika nchi za nje.