Wizara ya Ulinzi Tanzania: Tumejiweka tayari kukabiliana na ugaidi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i6901-wizara_ya_ulinzi_tanzania_tumejiweka_tayari_kukabiliana_na_ugaidi
Serikali ya Tanzania imesema kuwa hali ya ulinzi na usalama wa mipaka yote ya nchi hiyo ni shwari na kwamba imejipanga kukabiliana na wimbi la makundi ya kigaidi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 11, 2016 23:42 UTC
  • Wizara ya Ulinzi Tanzania: Tumejiweka tayari kukabiliana na ugaidi

Serikali ya Tanzania imesema kuwa hali ya ulinzi na usalama wa mipaka yote ya nchi hiyo ni shwari na kwamba imejipanga kukabiliana na wimbi la makundi ya kigaidi.

Hayo yamesemwa na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ingawa wizara hiyo imetaka kupatiwa fedha zaidi za bajeti. Waziri wa Ulinzi Dakta Hussein Mwinyi ameongeza kuwa wizara yake imejiimarisha kwa mikakati thabiti ya kukabiliana na tatizo la matukio ya ugaidi yanayoendelea katika nchi jirani, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha inazuia misimamo ya kufurutu ada ya vijana nchini Tanzania. Akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa mwaka wa fedha 2016/17, Waziri Mwinyi amelalamikia hali ya kutengewa bajeti ndogo na kupatiwa fedha pungufu na kusema hali hiyo imekuwa ikiathiri utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya jeshi na kusababisha ulimbikizwaji wa madeni hususan ya kimikataba. Ameongeza kuwa pamoja na changamoto hizo, jeshi la Tanzania limeendelea kujiimarisha na kulinda mipaka ya nchi ikiwa ni pamoja na kushughulikia changamoto zinazojitokeza kukiwemo kukabiliana na matukio ya uhalifu na viashiria vya machafuko kutoka nchi jirani. Amesisitiza kuwa hali ya mipaka ya Kaskazini, Mashariki, Magharibi na Kusini ni shwari, isipokuwa katika mpaka wa Magharibi ambao umekuwa ukishuhudia wakimbizi kutokana na machafuko ya kisiasa yanayoendelea katika nchi jirani ya Burundi. Amekiri kuwa hali ni tete katika ukanda wa Afrika Mashariki kutokana na matukio ya kigaidi yanayofanywa na vikundi vya kigaidi vya al-Shabaab na kusisitiza kuwa jeshi hilo limejipanga kufuatilia mienendo ya makundi hayo.