Hujuma dhidi ya Harakati ya Kiislamu Nigeria zimewafanya mayatima watoto 1,800
(last modified Sun, 25 Jul 2021 11:26:15 GMT )
Jul 25, 2021 11:26 UTC
  • Hujuma dhidi ya Harakati ya Kiislamu Nigeria zimewafanya mayatima watoto 1,800

Jukwaa la Akademia la Harakati ya Kiislamu ya Nigeria (IMN) limesema hatua ya vyombo vya usalama vya nchi hiyo kuhujumu na kushambulia shughuli za kidini za harakati hiyo imepelekea watoto karibu elfu mbili kuwa mayatima.

Katibu wa jukwaa hilo, Abdullahi Muhammad Musa amesema katika kikao na waandishi wa habari mjini Abuja kuwa, watoto 1,866 wamebaki kuwa mayatima baada ya utawala wa Rais Muhammadu Buhari kushambulia shughuli ya kidini katika mji wa Zaria mwaka 2015.

Amebainisha kuwa, serikali ya Buhari imepiga mnada mamlaka ya kujitawala nchi hiyo, kutokana na namna inavyoshirikiana na watawala wa Saudi Arabia kumdhalilisha na kumkandamiza Sheikh Ibrahim Zakzaky, kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria. 

Katibu wa Jukwaa la Akademia la Harakati ya Kiislamu ya Nigeria amesema ithibati kuwa kuna mkono wa Riyadh katika ukandamizaji wa Waislamu wa Kishia nchini Nigeria ni majivuno ya Mrithi wa Ufamle za Saudia, Muhammad Bin Salman katika mahojiano na gazeti la Time Magazine mnamo April 5, 2018.

Picha zinazoashiria ukubwa wa jinai ya Zaria

Katika mahojiano hayo, Bin Salman alijipiga kifua kwa kiburi akidai kuwa utawala wa Aal-Saud umefanikiwa kumkandamiza Sheikh Zakzaky kwa lengo la kusimamisha ushawishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Mwaka 2015 jeshi la Nigeria lilivamia shughuli za kidini katika Husseiniya ya Baqiyatullah katika mji wa Zaria na kuua karibu wafuasi elfu mbili wa Sheikh Zakaky waliokuwa wamekusanyika katika eneo hilo la ibada, mbali na kumtia nguvuni kiongozi huyo wa Kiislamu na mkewe ambao wanazuiliwa hadi hii leo.