Aug 03, 2021 03:16 UTC
  • Makumi wapoteza maisha katika ajali ya barabarani Kongo DR

Makumi ya watu wamepoteza maisha katika ajali mbaya ya barabarani iliyotokea huko magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Kapteni wa Polisi ya DRC, Antoine Pululu aliliambia shirika la habari la AFP jana Jumatatu kuwa, watu wasiopungua 33 wameaga dunia katika ajali hiyo iliyotokea usiku wa kuamkia Jumapili magharibi mwa nchi.

Amesema moto mkubwa ulizuka baada ya lori la mafuta kugongana ana kwa ana na basi lililokuwa limejaza abiria kupita kiasi katika kijiji cha Kibuba, umbali wa kilomita 80 kutoka mji mkuu Kinshasa.

Afisa mwingine wa polisi katika eneo hilo amesema miili ya wahanga wa ajali hiyo iliteketezwa na moto hadi kubakia majivu, na kwamba mabaki yaliyopatikana yalizikwa jana Jumatatu.

Eneo la tukio la ajali

Idadi kubwa ya watu hupoteza maisha katika ajali za barabarani kila mwezi nchini DRC kutokana na kupindukia kasi, magari mabovu, kubeba abiria na mizigo ziada na hali mbaya ya barabara.

Oktoba mwaka 2018, watu 53 waliaga dunia katika ajali nyingine iliyohusisha lori la mafuta katika moja ya barabara kuu za kuelekea Kinshasa. Mwaka 2010, watu 230 walifariki dunia baada ya lori jingine la mafuta kupinduka nchini DRC.

 

 

Tags