Wafuasi wa chama cha upinzani Tanzania Chadema wakamatwa wakiimba "Mbowe sio gaidi"
(last modified Thu, 05 Aug 2021 12:33:39 GMT )
Aug 05, 2021 12:33 UTC
  • Wafuasi wa chama cha upinzani Tanzania Chadema wakamatwa wakiimba

Wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambacho ni chama kikuu cha upinzani Tanzania waliokuwa wamekusanyika nje ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya kuzuiwa kuingia ndani ya korti wamekamatwa na wanashikiliwa na Jeshi la Polisi.

Wafuasi  hao waliokuwa wamefika mahakamani hapo kwa ajili ya kufuatilia kesi ya Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe ambaye hata hivyo hakufikishwa mahakamani walikamatwa baada ya kutoa mabango yenye jumbe mbalimbali na ktoa nara kuwa "Mbowe sio gaidi."

Askari waliokuwa kwenye magari mawili waliteremka kisha kuwazunguka na kuwakamata baadhi yao na wengine kufanikiwa kukimbia. Mbowe alifikishwa Mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Julai 26, 2021 kwa mashtaka mawili likiwemo la tuhuma za ugaidi.

Wakati huo huo, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imeshindwa kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Mbowe na wenzake watatu, baada ya teknolojia ya mtandano kwa njia ya video kuleta hitilafu. Kesi hiyo imeahirishwa hadi kesho Ijumaa Agosti 6.

 

Mbowe mikononi mwa maafisa usalama wa Tanzania

Kabla ya hapo, Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Amnesty International limesema kuwa, serikali ya Tanzania inapaswa kutoa ushahidi wa kesi dhidi ya kiongozi wa chama kikuu cha upinzani Tanzania Freeman Mbowe na ikishindwa kufanya hivyo basi iamuachie huru.

Kiongozi huyo wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini Tanzania, alitiwa mbaroni alfajiri ya kuamkia Julai 21 akiwa katika hoteli ya Kingdom mtaa wa Ghana alikokifikia kwa ajili ya kushiriki kongamano la Katiba Mpya lililoandaliwa na Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha). Hata hivyo, siku iliyofuata Msemaji wa Polisi nchini humo, David Misime aliueleza umma kuwa Mbowe anakabiliwa na tuhuma mbalimbali ikiwemo za kupanga njama za kufanya vitendo vya kigaidi na kuua viongozi wa Serikali.