Kwa akali watu 15 wauawa katika milipuko miwili ya mabomu nchini Somalia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i73380-kwa_akali_watu_15_wauawa_katika_milipuko_miwili_ya_mabomu_nchini_somalia
Kwa akali watu 15 wanaripotiwa kuuawa nchini Somalia na makumi ya wengine kujeruhiwa kufuatia shambulio la kigaidi la milipuko miwili ya mabomu katika eneo moja katikati mwa nchi hiyo.
(last modified 2025-11-16T06:33:27+00:00 )
Aug 11, 2021 07:41 UTC
  • Kwa akali watu 15 wauawa katika milipuko miwili ya mabomu nchini Somalia

Kwa akali watu 15 wanaripotiwa kuuawa nchini Somalia na makumi ya wengine kujeruhiwa kufuatia shambulio la kigaidi la milipuko miwili ya mabomu katika eneo moja katikati mwa nchi hiyo.

Duru za usalama kutoka nchini humo zinaripoti kuwa, mlipuko wa kwanza ulitokea katika eneo la Mudug katikati mwa Somalia ambapo watu wanane wakiwemo watoto watatu wenye umri wa chini ya miaka mitano waliuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa.

Aidha taarifa zaidi zinasema kuwa, watu wengine saba wameuawa katika mlipuko wa pili wa bomu uliotokea katika eneo la Shabelle lililoko kusini mwa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Ripoti zinasema kuwa, waliouawa katika mlipuko wa pili ni askari wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika AMISOM.

Wanamgambo wa al-Shabab nchini Somalia

 

Kundi la kigaidi la al-Shabab limetangaza kuwa, wanachama wake wamehusika katika mlipuko wa bomu wa pili dhidi ya askari wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika AMISOM.

Hivi karibubni jeshi la Somalia likishirikiana na askari wa  askari wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika AMISOM lilifanikiwa kuukomboa mji wa kistratajia wa Janale ulioko kwenye eneo la Lower Shabelle, kusini mwa Somalia, toka mikononi mwa al-Shabab.

Tangu mwaka 2007, kundi la kigaidi la al-Shabaab lenye mfungamano na mtandao wa al Qaida limekuwa likifanya mashambulizi ndani ya Somalia kwa lengo la kuiangusha serikali kuu ya nchi hiyo inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika.