12 wauawa katika mapigano baina ya wavuvi na wachungaji Cameroon
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i73468-12_wauawa_katika_mapigano_baina_ya_wavuvi_na_wachungaji_cameroon
Kwa akali watu 12 wameuawa huku makumi ya wengine wakijeruhiwa katika mapigano baina ya wavuvi na wachungaji wa mifugo huko kaskazini mwa Cameroon.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 13, 2021 08:36 UTC
  • 12 wauawa katika mapigano baina ya wavuvi na wachungaji Cameroon

Kwa akali watu 12 wameuawa huku makumi ya wengine wakijeruhiwa katika mapigano baina ya wavuvi na wachungaji wa mifugo huko kaskazini mwa Cameroon.

Hayo yalisemwa jana Alkhamisi na Gavana wa eneo la Far North la kaskazini mwa Cameroon, Midjiyawa Bakari ambaye ameeleza kuwa, mauaji hayo yalitokea baada ya pande mbili hizo kuzozana kutokana na sababu zisizo na maana katika wilaya za Logone na Chari katika eneo hilo lililoko mpakani na Chad na Nigeria.

Amesema mbali na watu 12 kuuawa katika mapigano hayo, wengine 48 wamejeruhiwa na kulazwa katika hospitali ya Kousseri nchini Cameroon huku wengine wakipelekwa jijini N'Djamena nchini Chad kwa ajili ya matibabu.

Agosti 7 katika nchi hiyo jirani ya Chad, mzozo mwingine baina ya wafugaji na wavuvi ulipelekea watu 22 kuuawa, huku wengine 18 wakijeruhiwa.

Mapigano baina ya wavuvi, wakulima na wafugaji yanashuhudiwa sana Afrika Magharibi

Mwishoni mwa mwezi uliopita, wanajeshi wasiopungua saba wa Cameroon waliuawa baada ya wanachama wa kundi la kigaidi la Boko Haram kushambulia kambi moja ya kijeshi katika eneo hilo la kaskazini mwa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Duru za kiusalama zinaarifu kuwa, watu zaidi ya 2,000 wameuawa tangu genge hilo la ukufurishaji lianzishe harakati na mashambulio yake katika eneo la Far North la kaskazini mwa Cameroon mwaka 2014.