Serikali ya Burundi yasema itashiriki mazungumzo ya amani Tanzania
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i7396-serikali_ya_burundi_yasema_itashiriki_mazungumzo_ya_amani_tanzania
Serikali ya Burundi imesema, itahudhuria mazungumzo ya amani ya nchi hiyo yaliyopangwa kufanyika mjini Arusha, Tanzania kwa usuluhishi wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EAC).
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 19, 2016 23:37 UTC
  • Serikali ya Burundi yasema itashiriki mazungumzo ya amani Tanzania

Serikali ya Burundi imesema, itahudhuria mazungumzo ya amani ya nchi hiyo yaliyopangwa kufanyika mjini Arusha, Tanzania kwa usuluhishi wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EAC).

Mazungumzo hayo yanatazamiwa kufanyika mwishoni mwa wiki kwa lengo la kuhatimisha mlolongo wa machafuko, mapigano na mauaji ya mwaka mmoja ambayo yamesababisha watu wapatao 450 kuuawa na kuacha mamia ya maelfu ya wengine wakilazimika kuyahama makazi yao na kuwa wakimbizi.

Mazungumzo ya amani ya Burundi yameakhirishwa mara kadhaa tangu yalipofanyika kwa mara ya kwanza mwezi Desemba mwaka jana kutokana na serikali ya Bujumbura kukataa kukaa meza moja na yale inayodai ni makundi ya uasi.

Duru ijayo ya mazungumzo hayo imepangwa kufanyika siku ya Jumamosi mjini Arusha, kaskazini mwa Tanzania kwa usuluhishi wa rais wa zamani wa nchi hiyo Benjamin Mkapa kwa niaba ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Msemaji wa serikali ya Burundi Willy Nyamitwe, amesema kizuizi hicho bado kingalipo lakini ameongeza kuwa wamepokea mwaliko na kwa hivyo watakwenda Arusha kushiriki mazungumzo hayo.

Mgogoro wa kisiasa nchini Burundi ulizuka mwezi Aprili mwaka uliopita wa 2015 wakati rais wa nchi hiyo Pierre Nkurunziza alipotangaza kuwa atagombea urais kwa mara ya tatu, uamuzi ambao wapinzani wake walisema ulikiuka katiba ya nchi hiyo.../