Rais wa Zambia awafuta kazi wakuu wa vyombo vya usalama
(last modified Mon, 30 Aug 2021 11:28:31 GMT )
Aug 30, 2021 11:28 UTC
  • Rais wa Zambia awafuta kazi wakuu wa vyombo vya usalama

Rais mpya wa Zambia, Hakainde Hichilema ameanza kazi kwa kasi kubwa; ambapo amewapiga kalamu nyekundu makamanda wakuu wa jeshi, sanjari na kuwabadilisha wakuu wa Idara ya Polisi ya nchi hiyo.

Katika hotuba yake kwa taifa kwa njia ya televisheni, Hichilema ametangaza kuteua wakuu wapya wa jeshi la nchi kavu na lile la anga la nchi hiyo, huku pia akiteua mkuu wa kitengo kipya cha ulinzi.

Pasi na kutoa sababu za uamuzi wake huo, Rais mpya wa Zambia ambaye alikula kiapo cha kulitumikia taifa wiki iliyopita ameongeza kuwa, "nimewafuta kazi makamishna wote wa polisi."

Kadhalika ametoa onyo kali kwa jeshi la polisi la nchi hiyo akisema: Hakuna yeyote anayepaswa kukamatwa kabla ya uchunguzi kukamilika.

Maafisa usalama  wa Zambia

Hichilema ni muhanga wa utumiaji mabavu na mbinyo wa vyombo vya usalama, kwani katika utawala uliopita wa Edgar Lungu, alitiwa mbaroni mara zaidi ya 12 bila sababu zisizo na msingi.

Mwanasiasa huyo aliahidi kulifanyia mabadiliko makubwa jeshi la polisi la nchi hiyo wakati wa kampeni za kugombea urais iwapo ataibuka mshindi.

Hakainde Hichilema wa chama cha United Party for National Development (UPND) alipata kura 2,810,777 akimpita kwa mbali Edgar Lungu wa chama cha Patriotic Front (PF) aliyepata kura 1,814,201. Hiyo ilikuwa mara ya sita kwaHichilema kuwania urais.