Bakwata yalaani rasmi shambulio la msikitini mjini Mwanza, Tanzania
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i7537-bakwata_yalaani_rasmi_shambulio_la_msikitini_mjini_mwanza_tanzania
Baraza Kuu la Waislamu Tanzania, (Bakwata) limelaani mauaji ya hivi karibuni yaliyofanywa na watu wanaodhaniwa kuwa wakufurishaji katika msikiti mmoja jijini Mwanza.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 21, 2016 23:51 UTC
  • Bakwata yalaani rasmi shambulio la msikitini mjini Mwanza, Tanzania

Baraza Kuu la Waislamu Tanzania, (Bakwata) limelaani mauaji ya hivi karibuni yaliyofanywa na watu wanaodhaniwa kuwa wakufurishaji katika msikiti mmoja jijini Mwanza.

Mufti na Shehe Mkuu Abubakari Zubeir, imewataka Waislamu kuwa watulivu sanjari na kutoa ushirikiano kwa vyombo vya usalama ili kuwabaini wahalifu wa jinai hiyo iliyopelekea watu watatu kuuawa na wengine kujeruhiwa, wanakamatwa na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria. Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mauaji hayo yaliyotokea Jumatano saa mbili usiku wakati waumini hao wakiswali swala ya Isha, sheikhe Zubeir alisema tukio hilo la watu wasiojulikana kuvamia na kuwaua waumini msikitini ni la kinyama ambalo halipaswi kuvumiliwa. Alisema na hapa ninamnukuu: “Kwa niaba ya Bakwata tunalaani vikali tukio hili pamoja na kuwataka Waislamu kuwa watulivu katika kipindi hiki kigumu. Lakini pia nawaomba Waislamu na wananchi kwa ujumla kuvipa ushirikiano vyombo vyetu vya usalama ili wahalifu hawa wapatikane.” Mwisho wa kunukuu. Aidha alisema Uislamu ni dini ambayo moja ya misingi yake ni kulinda nafsi kama anavyofundisha Mwenyezi Mungu katika Kitabu Kitakatifu cha Qurani na kuongeza kuwa, baraza hilo linawapa pole wafiwa wote pamoja na waumini wa Masjid Rahmaan kwa msiba huo. Kwa mujibu wa mashuhuda, watu waliovamia msikiti huo na kufanya jinai hiyo, walikuwa na bendera za kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh, suala linalothibitisha kuwepo mkono wa matakfiri hao katika tukio hilo.