UN: Makubaliano ya amani ya Sudan Kusini yako hatarini
(last modified Thu, 09 Dec 2021 04:32:56 GMT )
Dec 09, 2021 04:32 UTC
  • UN: Makubaliano ya amani ya Sudan Kusini yako hatarini

Umoja wa Mataifa umeonya kuwa, makubaliano ya amani yaliyofikiwa mwaka 2018 nchini Sudan Kusini yapo katika hatari kubwa kutokana na mwendo wa kinyonga wa kuyatekeleza.

Indhari hiyo ilitolewa jana Jumatano jijini Juba na Nicholas Haysom, Mjumbe Maalumu wa Katika Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Sudan Kusini, ambaye pia ni mkuu wa ofisi ya UN katika nchi hiyo changa ya Afrika.

Amebainisha kuwa, pamoja na kuwa anapongeza hatua zilizopigwa na pande za kisiasa nchini humo tangu mapatano hayo ya amani yasainiwe, lakini haridhishwi na mwendo wa kobe wa kutekelezwa kwake.

Afisa huyo wa UN nchini Sudan Kusini ameongeza kuwa, makubaliano hayo yanapaswa kutekelezwa kwa maslahi ya wananchi wa Sudan Kusini wenyewe, huku akisisitiza kuwa hayana mfungamano wowote na nchi za kigeni.

Mahasimu wa kisiasa na kiuongozi Sudan Kusini wamesaini makubaliano ya amani mara kadhaa

Martin Elia Lomoro, Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan Kusini hata hivyo anadai kuwa, kutotekelezwa mapatano hayo kwa mwendo wa kasi uliotarajiwa kunatokana na uhaba wa fedha za kufanikisha mchakato huo.

Sudan Kusini ndiyo taifa changa zaidi Afrika baada ya kujitenga na Sudan na kuwa nchi huru mnamo 2011. Vita vya ndani nchini humo vilivyoanza Disemba 2013 vimeshababisha mauaji ya maelfu ya watu na kulazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi.