Dec 25, 2021 08:42 UTC
  • DRC yaangamiza ugonjwa wa meningitis Tshopo

Hatimaye Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC imetangaza kuwa mlipuko wa ugonjwa wa homa ya uti wa mgongo au meningitis katika jimbo la Tshopo kaskazini-mashariki mwa nchi hiyo, umetokomezwa.

Taarifa iliyotolewa Ijumaa na Shirika la Afya Duniani, WHO jijini Kinshasa, DRC na Brazaville, Jamhuri ya Congo imesema tangazo hilo linazingatia kwamba katika siku 42 hakuna mgonjwa mpya aliyethibitika kuwa na maambukizi ya ugonjwa huo tangu mgonjwa wa mwisho aruhusiwe kutoka hospitalini.
Mafanikio ya kutokomeza ugonjwa huo yanafuatia ushirikiano wa karibu na thabiti kati ya WHO na mamlaka za afya za kitaifa na kijimbo nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.
Mlipuko huo wa homa ya uti wa mgongo jimboni Tshopo uliripotiwa tarehe 7 mwezi Septemba mwaka huu wa 2021 ambapo hadi kutokomezwa umesababisha vifo vya watu 205 kati ya wagonjwa 2662.
Hatua zilizochukuliwa hadi kutokomeza ugonjwa huo ni pamoja na ufuatiliaji wa wagonjwa, utoaji wa chanjo  huduma ambazo zilifanyika kwenye vituo na pia kwa kutumia magari yaliyofikia wananchi kokote waliko, hatua ambazo ziliwezesha kupunguza kiwango cha vifo miongoni mwa wagonjwa kutoka asilimia 85 hadi asilimia 10 katika kipindi cha chini ya wiki moja.
Akizungumzia ugonjwa wa homa ya uti wa mgongo, Mkurugenzi wa WHO kanda ya Afrika Dkt. Matshidiso Moeti amesema “ni hatari, unaingia haraka mwilini na unaua. Kutokomeza ugonjwa wa homa ya uti wa mgongo katikati ya mazingira magumu ya sasa ya ugonjwa wa Corona au COVID-19 si jambo rahisi kwa mamlaka. Lakini ni lazima tuwekeze zaidi ili kuweza kubaini, kuzuia na kupunguza madhara ya ugonjwa huu wa homa ya uti wa mgongo.”
Ugonjwa wa homa ya uti wa mgongo ni ugonjwa unasababishwa na bakteria na huambukizwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine kupitia majimaji ya mwilini. Mgonjwa aliyeambukizwa anaweza kufa ndani ya saa chache na hadi sasa ugonjwa huu ni changamoto kubwa kwa afya ya umma.

Tags